2565; Ni juhudi zipi ambazo umeweka?

Kuna kitu unachotaka, lakini vikwazo na changamoto zinakuzuia usipate kitu hicho.

Ni rahisi kutumia hiyo kama sababu ya kukosa unachotaka, na kujifariji kwamba hakuna namna.

Kabla hujaendelea kujifariji, nikukumbushe kitu kimoja muhimu, hakuna aliyefanya makubwa ambaye hakukutana na vikwazo na changamoto.

Kwa hakika, pale tu unapoamua kufanya makubwa, unakuwa umeziambia changamoto njooni kwangu.

Kwa hiyo kama unafikiri kuna njia ya kuweza kufanya makubwa isiyokuwa na vikwazo na changamoto, unajidanganya.

Hivyo basi, jambo la msingi siyo kama kutakuwa na changamoto au la, uhakika ni zitakuwepo. Jambo la msingi ni unafanya nini.

Ni juhudi zipi ambazo unaweka kwenye kile unachotaka, licha ya vikwazo na changamoto zilizopo?
Maama hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuvuka hayo na kupata unachotaka.

Malalamiko, sababu, visingizio na kujifariji hakutakupa chochote unachotaka. Hizo ni njia za kujisumbua tu na kukwepa kuweka juhudi.

Kama kweli unataka kupata unachotaka, weka hayo mengine yote pembeni na uweke juhudi kubwa kwenye kile ulichochagua kufanya.

Juhudi ziwe endelevu na siyo za kukariri, bali ujitathmini na kisha uboreshe zaidi juhudi unazoweka.

Hakuna juhudi unazoweka zikapotea. Hata kama huoni matokeo yake sasa, yatakuja kuonekana tu baadaye.
Hivyo usiangalie sana matokeo kwa sasa, wewe angalia ni juhudi zipi sahihi unazoweka.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila sababu unayojipa kwa nini hujafika unakotaka au kupata unachotaka, jiulize ni juhudi zipi ambazo umekuwa unaweka. Maneno bila juhudi ni kujilisha upepo. Juhudi za kawaida na za mazoea ni kujifanganya tu.
Ni lazima uweke juhudi za makusudi ili uweze kupata makubwa unayotaka.

Tafakari;
Mafanikio yangekuwa rahisi, kila mtu angekuwa nayo na isingekuwa kitu kinachozungumziwa sana. Mafanikio makubwa kwenye eneo lolote lile ni magumu, yana vikwazo na changamoto. Lakini dawa ya yote hayo ipo, ambayo ni juhudi zinazowekwa. Hakuna kikwazo au changamoto inayoweza kushinda juhudi zinazowekwa bila kuchoka.

Kocha.