2567; Kwa sababu wengine wanafanya.

Sisi binadamu tunashawishiwa sana na binadamu wengine kuliko kitu kingine chochote.
Ni rahisi sana kufanya kile ambacho wengine wanafanya, hata kama umejiambia hutafanya.

Mambo yote, mazuri na mabaya huwa yanafanyika kwa sababu hiyo. Pale mtu anapoona wengine wanafanya, basi anaona siyo vibaya na yeye akifanya.

Kaa na walevi na haitakuchukua muda mrefu kabla na wewe hujaanza kunywa, hata kama ulijiambia hutatumia vilevi.

Kaa na watu waliokata tamaa na haitakuchukua muda mrefu na wewe utakuwa umekata tamaa, hata kama ulikuwa na matumaini makubwa kiasi gani.

Usidharau nguvu ya ushawishi wa watu, habari, sinema, mitandao na vitu vingine. Vyote hivyo vina nguvu ya kukubadili wewe kwa namna fulani.

Hivyo kama hutaki mabadiliko yasiyo sahihi kwako, kama hutaki kutoka kwenye msingi wako, kuwa makini sana na wale unaowachagua kushirikiana nao au kuwa nao karibu.
Ni rahisi kufanya yale wanayofanya wengine, kuliko kufanya unayopanga wewe. Zungukwa na watu sahihi, ili hata unapowaiga, basi uwe umeiha yaliyo sahihi.

Na kwa upande wa pili, jua kila unachofanya, unawashawishi wengine nao wafanye. Kama hutaki kuwa na ushawishi mbaya, fanya yaliyo sahihi.

Hatua ya kuchukua;
Kagua watu wote unaojihusisha nao kwa karibu na ujue tabia na mitazamo yao, kwa sababu hivyo ndivyo utakavyoishia kuwa navyo.
Angalia aina ya maisha waliyonayo na jua hayo ndiyo maisha utakayokuwa nayo pia.
Kama unataka matokeo ya tofauti, badili watu ambao unatumia nao muda wako mwingi.

Tafakari;
Pamoja na uwezo mkubwa tulionao binadamu, bado ushawishi wa wengine una nguvu kubwa sana kwetu. Tusidharau nguvu hiyo wala kupingana nayo, bali tuitumie kwa manufaa yetu.

Kocha.