#SheriaYaLeo (72/366); Jiboreshe kupitia kushindwa.

Kukosea na kushindwa ni zawadi kubwa kwako.
Kwani kunakuonyesha ni maeneo gani ambayo una madhaifu au bado hujawa imara kama inavyohitajika.

Unapofanya kitu na ukakosea au ukashindwa, haimaanishi kwamba huwezi kamwe kukifanya. Bali inamaanisha kuna vitu bado hujavijua katika kufanya kitu hicho.
Hivyo unapaswa kujifunza kwa kina kupitia makosa na kushindwa kwako na kufanya tena kwa ubora zaidi.

Kwenye biashara na ujasiriamali hili ni muhimu zaidi. Mara nyingi huwezi kujua kipi sahihi au siyo sahihi na kipi ni muhimu au siyo muhimu.
Lakini mwitikio wa soko huwa upo wazi kabisa. Soko litakuonyesha kipi ni sahihi na kipi siyo, kipi ni muhimu na kipi siyo.

Kila aliyefanikiwa, hakuanza akiwa anajua kila kitu, bali alienda akikosea na kujiboresha zaidi.
Na wewe pia tumia njia hii, ukishaamua kile unachotaka, ukishajua ubobezi wa juu unaotaka kufikia, jua kila kitu kwako ni darasa.
Kila matokeo unayoyapata, yawe mazuri au mabaya yana funzo kwako kuhusu nini ni muhimu na nini siyo muhimu, nini ni sahihi na nini siyo sahihi.

Tumia makosa na kushindwa kwako kama darasa la kujiboresha zaidi kwenye safari yako ya mafanikio.
Kila unapokosea au kushindwa usikate tamaa na kuona haiwezekani, bali ichukue kama fursa ya kujifunza na itumie kuwa bora zaidi.

#SheriaYaLeo; Kukosea na kushindwa ni njia ya kujifunza. Ni vitu vinavyojaribu kukupa taarifa muhimu. Unapaswa kuvitumia ili kuwa bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji