2571; Machache kabla ya mengi.

Mawazo unayoweza kuyafanyia kazi ni mengi.
Fursa unazoweza kunufaika nazo ni chungu mzima.

Lakini kuna ukomo wa rasilimali muhimu kama muda, nguvu na fedha.

Ukomo huo unakutaka uweke vizuri vipaumbele vyako ili uweze kuzitumia rasilimali hizo vizuri.

Lakini wengi wamekuwa wanashindwa na hilo, wanashindwa kuweka vipaumbele na kujikuta wakihangaika na mambo mengi.

Mwisho wanashangaa kwa nini hawapigi hatua licha ya kuhangaika na mengi.

Kabla hujahangaika na mengi, hebu kwanza hangaika na machache na uweze kuyafanyia kazi vizuri kabisa.
Hakikisha hayo machache umeyafanya kwa kina mpaka kuweza kupata matokeo mazuri.

Ukishayaweza machache, ndiyo unaweza kwenda kwenye mengi.
Lakini kukimbilia mengi wakati machache bado yanakusumbua, ni kujipoteza zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila mawazo na fursa nzuri unazopata za kufanya, andika pembeni na jiambie utaanza kufanyia kazi baada ya kukamilisha kwa kina yale unayofanyia kazi sasa.
Kwa njia hiyo utaacha kusumbuka na fursa mpya za kila wakati.

Tathmini;
Rasilimali zenye ukomo zinapaswa kupangiliwa na kutumiwa vizuri ili ziweze kuwa na tija. Ukizitawanya tu hovyo kwa kila kinachojitokeza mbele yako, utazipoteza na usipate manufaa.

Kocha.