2575; Mabadiliko makubwa hayaletwi na wengi.
Mabadiliko makubwa kabisa hayajawahi kuletwa na watu wengi.
Bali huwa ni matokeo ya watu wachache waliojitoa kweli ili kuhakikisha wanakamilisha wanachotaka.
Ni vigumu sana kwa watu walio wengi kuweza kukitoa kwa muda mrefu bila kuchoka.
Kundi la watu wengi huwa ni rahisi kupotea kwa kutaka kumridhisha kila mtu.
Kundi la watu wengi linaenda kwa kubembelezana sana ili wingi huo uendelee kuwepo.
Kwenye kundi la wachache vikwazo hivyo havipo.
Wachache wanaweza kujitoa kwa muda mrefu bila kuchoka.
Wachache tayari wana msukimo ndani yao hivyo hawahitaji kubembelezwa sana.
Hatua ya kuchukua;
Kama kuna mabadiliko makubwa unayotaka kuyaleta kwenye eneo lolote lile, jua huhitaji watu wengi, bali wachache waliojitoa kweli kweli.
Hivyo wajibu wako ni kuwatafuta hao wachache, kuwapa maono yako, kisha kwa pamoja muyafanyie kazi mpaka kuyafikia.
Usiangalie sana wingi wa watu, bali angalia ni kwa namna gani wamejitoa.
Tafakari;
Mabadiliko ni magumu sana kuletwa na wengi kwa sababu nguvu kubwa inatumika kuwaweka pamoja hao wengi kuliko kupambania mabadiliko.
Kama kinachohitajika ni mabadiliko kwa matokeo, wachache waliojitoa kweli wanatosha.
Kocha.