Rafiki yangu mpendwa,

Tukianza na ukweli usiopingika ni kwamba huwezi kuwa Elon Musk, tajiri namba moja duniani katika kipindi hiki ninachoandika hapa (2022).

Lakini kuna mambo unaweza kujifunza kwake na yakaibua hamasa na msukumo kwako wa kuweza kufanya makubwa na kupata mafanikio.

Elon Musk amekuwa tofauti sana na mabilionea wengine kwa sababu ameweza kuleta mapinduzi kwenye tasnia tatu tofauti.

Ameleta mapinduzi kwenye tasnia ya magari ya umeme kupitia kampuni yake ya Tesla.

Ameleta mapinduzi kwenye usafiri wa kwenda angani kupitia kampuni yake ya SpaceX.

Pia ameleta mapinduzi kwenye umeme jua kupitia kampuni yake ya Solar City.

Na hapo hatujaweka kwamba alianzia kwenye kampuni iliyoleta mapinduzi kwenye kutuma na kupokea fedha mtandaoni, PayPal.

Swali ambalo wengi wamekuwa wanajiuliza ni je Musk amewezaje yote hayo?

Mwandishi na mwanasayansi Alexey Guzey ameandika makala ambayo ameainisha sifa sita ambazo Elon Musk anazo kwa pamoja, ambazo ni ngumu sana kuzikuta kwa mtu mmoja.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha sifa hizo sita kisha wewe mwenyewe uone kama unaweza kujijengea sifa hizo na uweze kufanya makubwa kwenye eneo lolote ulilochagua.

Ili uwe Elon Musk, unahitaji uwe na uwezo wa juu sana kuliko watu wengine wote (99th percentile) kwenye maeneo haya sita.

1. Nguvu.

Unahitaji kuwa na nguvu za juu kabisa za kuweza kuweka kazi ya uhakika na ya muda mrefu ndiyo uweze kupata mafanikio makubwa.

Elon Musk yuko kwenye tasnia ya teknolojia tangu mwaka 1995 na amekuwa akifanya kazi mpaka leo.

Wakati watu wengine wanafanya kazi masaa 40 kwa wili, Elon huwa anafanya kazi mpaka masaa 120 kwa wiki. Mara tatu ya mtu wa kawaida!

Mahali pamoja Elon amewahi kusema kama watu wanafanya kazi masaa 40 kwa wiki na wewe ukafanya masaa 100, lazima utazalisha mara mbili yao.

Bila kusahau Elon hajachukua likizo kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Hiyo ni baada ya kuugua malaria kali kwenye likizo yake moja na kujiambia kuchukua likizo ni kutafuta kifo.

Swali kwako; Je unawesa kufanya kazi mara mbili ya watu wanavyofanya kwa kawaida na kwa muda mrefu zaidi ya wengine bila kuishia njiani?

2. Ung’ang’anizi.

Elon amekuwa tajiri namba moja duniani mwaka 2021. Lakini amekuwepo kwenya tasnia ya teknolojia kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Amekutana na magumu na changamoto mbalimbali.
Kuna wakati makampuni yake yalitaka kufilisika, lakini akapambana mpaka kuyaokoa.

Kwa kipindi chote amekuwa aking’ang’ana bila ya kukata tamaa.

Swali kwako; je upo tayari kung’ang’ana na kile unachotaka bila ya kukata tamaa licha ya kukutana na magumu?

3. Ubunifu na nguvu ya akili.

Wakati taasisi ya anga ya Marekani (NASA) ilikuwa ikishindwa kufanya safari za anga mara kwa mara, kampuni ya anga ya Elon (SpaceX) imeweza kuja kubadili hilo na kuweza kufanya safari nyingi za angani.

Kilichoikwamisha NASA ilikuwa ni fikra walizokuwa nazo kwamba roketi ilishaenda angani haiwezi kurudi na kutumika tena. Hivyo gharama za kwenda angani zikawa kubwa, kwa sababu kila mara roketi mpya ilibidi zitengenezwe.

SpaceX ilikuja kubadili hilo kwa kuweza kutengeneza roketi zinazoweza kwenda angani na kurudi kisha kutumika tena. Hilo lilipunguza sana gharama za kwenda angani na hivyo safari za angani zikawa nyingi.

Elon aliweza hilo kwa sababu ya msingi wake wa kufikiri anaouita First Principle Thinking.
Kwa msingi huu, kila kitu anakifikiria kama hakijawahi kufanyika.

Yaani badala ya kuangalia kitu jinsi kinavyofanyika sasa na kuanza kukifikiria hivyo, unapaswa kufikiria kitu kama vile hakijawahi kufanyika.

Kwa njia hiyo hutazuiwa na fikra au ukomo uliopo, bali utakuwa huru kufikiri na kuja na ubunifu mpya.

Hivyo ndivyo ubunifu na nguvu ya fikra vinavyoweza kuleta matokeo makubwa.

Swali kwako; je unatumiaje ubunifu wako na nguvu kubwa ya akili yako? Unafikiria kile kilichozoeleka au kufikiria vitu kwa upya?

4. Matamanio makubwa.

Elon amekuwa na malengo mengi makubwa, ambayo yamekuwa yanamsukuma kufanya yale anayofanya.
Lakini mara kwa mara amekuwa akishirikisha matamanio yake makubwa yanayomsukuma kufanya kazi kupitiliza.

Tamanio la kwanza ni kila gari duniani kuwa la umeme. Elon amekuwa anasema hilo wazi kwamba ataweka juhudi mpaka ahakikishe kile gari duniani ni la kutumia umeme.

Tamanio la pili ni binadamu kuweza kuishi kwenye sayari ya Mars. Elon amekuwa anasema kuitegemea dunia kuwa nyumbani kwetu pekee ni hatari kubwa kwetu binadamu. Kama itatokea hatari yoyote ya kuidhuru dunia, hatutakuwa na pa kukimbilia.
Hivyo anapambana kuhakikisha binadamu tunaweza kuwa na makazi nje ya dunia.

Swali kwako; je ni matamanio gani makubwa uliyonayo ambayo yanakusukuma kufanya makubwa na kuondoka kwenye mazoea?

5. Kuchukua hatari na kuvumilia maumivu.

Elon amekuwa anachukua hatari kubwa na kuvumilia maumivu anayokutana nayo kwenye safari yake.

Walipouza kampuni yao ya kwanza, Paypal, Elon alichukua fedha zote alizopata na kuziwekeza kwenye kampuni zake mpya.

Hii ni hatari kubwa kuchukua, kuwekeza fedha zote ambazo mtu unazo kwenye kampuni mpya yenye hatari ya kufa ni kitu ambacho siyo wengi wanaweza kufanya.

Kuna kipindi kampuni zake zilikaribia kufilisika, yaani ilibaki siku chache tu ziwe zimefilisika, lakini alipambana kwa kila namna mpaka kuziokoa zisifilisike.

Swali kwako; ni hatari zipi kubwa uko tayari kuchukua? Ni maumivu kiasi gani uko tayari kuyahimili katika kufanyia kazi ndoto zako?

6. Maono makubwa na mipango ya muda mrefu.

Kutaka magari yote duniani yawe yanatumia umeme siyo kitu kidogo na wala haitatokea haraka, itachukua muda mrefu.

Binadamu kuweza kuwa na makazi nje ya dunia siyo kitu kidogo na haitatokea kwa urahisi, itahitaji kazi na muda mrefu.

Japokuwa Elon amefikia utajiri namba moja duniani mwaka 2021, alianza muda mrefu juhudi zake, kwa karibu miaka 30, akiwa na maono makubwa na mipango ya muda mrefu anayoifanyia kazi bila kuchoka.

Swali kwako; ni maono yapi makubwa kabisa uliyonayo? Ni mipango gani ya muda mrefu unayofanyia kazi kila siku bila kukata tamaa?

Rafiki, kama nilivyotangulia kukuambia, huwezi kuwa Elon Musk, ila kuna mengi ya kujifunza kwake ili uweze kufanya makubwa.

Jipe majibu ya maswali sita niliyoshirikisha kwenye makala hii na yafanyie kazi majibu hayo kila siku bila kuchoka au kuishia njiani.
Hata kama hutakuwa bilionea, hata kama hutajulikana duniani, utakayofanya yatakuwa makubwa na yataacha alama kubwa.

Nikukaribishe ujipatie kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO ili uweze kujipa ubatizo muhimu sana unaohitaji ili ujitoe kweli kweli kufanikiwa.
Kwenye kitabu nimeshirikisha mfano wa Elon alivyokataa likizo na kuziona kama kifo na hilo limempa msukumo wa kuendelea kujituma zaidi.

Kama unataka kuachana na maisha ya kawaida. 
Kama unataka kuacha kwenda kwa mazoea.
Na kama unataka kuacha alama hapa duniani,
Jipatie leo na usome kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO.
Wasiliana na 0752 977 170 kupata nakala yako ya kitabu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr. Makirita Amani.