2584; Nyama zipo chini.
Maisha ni kama kunywa mtori,
Haijalishi utautikisa vipi,
Nyama utazikuta chini.
Ni lazima uunywe mtori wenyewe kwanza ndiyo uweze kuzifikia nyama.
Mtori ndiyo maisha yetu ya kila siku na nyama ndiyo kile tunachokitaka.
Watu wengi huhangaika na njia za mkato za kupata wanachotaka.
Lakini huishia kupoteza tu muda na fedha zao.
Kila unayemuona ambaye amepata anachotaka, kuna gharama kubwa amelipa kwenye muda, kazi na kuachana na mengine yasiyo na tija.
Ndiyo maana kanuni rahisi sana ya mafanikio ina hatua tatu;
Moja ni kujua kwa hakika nini hasa unachotaka. Kama hujui unachotaka, huwezi kukipata.
Mbili ni kujua gharama unayopaswa kulipa ili kupata unachotaka. Kila kitu kina gharama, hakuna cha bure.
Tatu ni kulipa gharama hiyo ili upate unachotaka. Bila kulipa gharama huwezi kupata unachotaka.
Hatua ya kuchukua;
Hata kama unajua hatua hizo tatu, chukua kalamu na karatasi na uziandike tena. Andika nini hasa unachotaka, gharama unayopaswa kulipa na namna unavyoilipa kila siku.
Tafakari;
Njia za mkato hazijawahi kuwa na matokeo mazuri zaidi ya kukuacha na mikato.
Njia za mkato zingekuwa zinafanya kazi zisingeitwa za mkato, bali zingekuwa ndiyo njia kuu.
Achana na njia za mkato, kunywa mtori wako taratibu, nyama utazikuta chini.
Kocha.