2589; Tarehe ya mwisho.

Elon Musk, bilionea namba moja duniani kwa sasa, amekuwa akijisukuma sana katika kuyaendesha makampuni yake, kitu ambacho kimeyafanya yawe na ufanisi mkubwa.

Katika kujisukuma huko amekuwa akijiwekea lengo na tarehe ya mwisho ya kulifikia.
Wakati mmoja alipata tenda ya serikali ya kufunga umeme wa jua na akaahidi atakamilisha kazi hiyo ndani ya siku 100 na ikizidi hata siku moja asilipwe.
Ilikuwa ni kazi kubwa na ambayo kwa kawaida ingechukua muda mrefu, lakini alipambana na kuikamilisha ndani ya muda.

Wakati mwingine aliahidi kabla ya mwaka kuisha kiwanda chake kingekuwa kimezalisha magari laki 5. Mwaka ukawa unakaribia kuisha na magari laki 5 hayajafikiwa.
Aliamua kuhamishia meza yake na godoro lake ndani ya kiwanda na akawa pale masaa 24 ya siku kwa siku zote 7 za wiki.
Kabla ya mwaka kuisha akawa amelifikia lengo.

Unapokuwa na tarehe ya mwisho ya kufanya au kukamilisha jambo, tarehe ambayo usipoizingatia utapata madhara makubwa, utajisukuma kwa kila namna kukamilisha ndani ya tarehe au muda huo.
Hutaruhusu sababu au kisingizio chochote kuingilia ufanyaji wako.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachopanga kufanya, jiweke ukomo wa muda na mwambie mtu au watu wanaoweza kukuwajibisha. Hilo litakusukuma uweze kukamilisha uliyopanga kwa wakati.

Tafakari;
Bila ukomo hakuna kinachotusukuma kwenda hatua ya ziada.
Jiwekee ukomo na uzingatie kweli ili uweze kufanya makubwa.

Kocha.