2592; Kula pipi na kubaki nayo.
Kutaka kula pipi na wakati huo huo kubaki nayo ndiyo kikwazo kikubwa kwa wengi kupata mafanikio makubwa.
Yaani mtu anataka apate ambacho hana, lakini pia hataki kupoteza alichonacho.
Hilo ni jambo lisilowezekana kwa namna yoyote ile, huwezi kupata ambacho huna bila kupoteza kile ambacho unacho.
Huwezi kupata matokeo makubwa kwa kuendelea kufanya vile unavyofanya sasa.
Huwezi kujenga tabia mpya nzuri bila ya kuvunja zile mbaya ulizonazo sasa.
Muda wako, nguvu zako na umakini wako ni rasilimali zenye uhaba mkubwa, ukishatumia kwenye eneo moja, huwezi kutumia tena kwenye eneo jingine.
Hivyo kila mara piga hesabu hiyo kali, ili kupata unachotaka unapaswa kupoteza nini ulichonacho?
Na nenda mbali zaidi na kujiuliza yale unayokumbatia sasa yanakuzuia kupata yapi muhimu zaidi?
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachotaka, jua kipi unapaswa kutoa na kitoe bila ya kusita.
Tafakari;
Kikwazo cha kwanza kwako kupata unachotaka ni kile ulichonacho sasa. Kuwa tayari kupoteza ulichonacho ili uweze kupata unachotaka.
Kocha.