2594; Rahisi kufanya.

Kitu ambacho ni rahisi kufanya huwa kinafanywa na watu wengi.

Kitu ambacho kinafanywa na watu wengi huwa kinakuwa na ushindani mkali.

Kitu chenye ushindani mkali huwa kinakuwa na faida kidogo.

Hii haimaanishi uende kufanya mapya kabisa.

Bali inamaanisha chochote unachofanya, hakikisha kuna namna unafanya ambavyo wengine hawawezi kufanya.

Kuna unafuu wa kufanya kile kinachofanywa na wengi, kwa sababu tayari kinaeleweka na kina wateja.

Wajibu wako ni kukifanya kwa namna ya kipekee, namna ambayo hakuna mwingine anafanya hivyo, ili watu wawe na sababu ya kuwaacha wengine na kuja kwako.

Kama huna kinachokutofautisha na wengine, kama hakuna kinachowafanya watu waache wengine na kuja kwako, hata watu ulionao ni kwa bahati tu.
Na kwa hakika watu hao siyo wako, kwani akitokea mwingine ni rahisi kukuacha na kwenda kwa huyo.

Hii ni kwenye kila eneo la maisha, kuanzia kazi, biashara, mahusiano na maisha kwa ujumla. Jua kinachokutofautisha na wengine na kitumie hicho kujenga upekee wako.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila eneo la maisha yako, tambua kile kinachokupa wewe upekee na kukutofautisha na watu wengine wote.
Fanya yale ambayo tayari yanafanyika, ila kwa namna ya kipekee kwako.
Hivyo ndivyo unavyojijengea uhodhi wako binafsi.

Tafakari;
Dunia inakulazimisha uwe kama wengine, ili usiwe ghali na uweze kutawalika kirahisi.
Wajibu wako ni kuwa wewe, ili uwe huru na asiwepo wa kukutawala bila matakwa yako.
Uwezo huo tayari upo ndani yako, ni wewe tu kuanza kuutumia.

Kocha.