2595; Kitakachomfaa kila mtu.
Ukitaka kuwa na kitu kitakachomfaa kila mtu, utaishia kuwa na kitu kisichomfaa yeyote.
Hebu fikiria kama mvua na jua vingekuwa vinawaka na kunyesha kwa kuendana na matakwa ya watu.
Nakuhakikishia kusingekuwa na majira yoyote.
Maana sehemu moja pangekuwa na mvua na jua kwa wakati mmoja, maana matakwa ya watu yanatofautiana.
Jua na mvua haviendi na matakwa ya watu, bali watu wanafanya matakwa yao yaendane na mpango wa mvua na jua, ambao upo nje ya uwezo wako.
Kwenye kazi na biashara yako, unaweza kushawishika sana uwe na bidhaa au huduma itakayomfaa kila mtu, ili usipoteze mteja yeyote.
Lakini hilo huwa halileti matokeo mazuri, kwani mwishowe unaishia na bidhaa au huduma isiyomfaa yeyote na hivyo kukosa wateja kabisa.
Ni lazima uchague kabisa kile unachofanya au kuuza kinawafaa watu wa aina gani.
Na hapo unakuwa pia umechagua kwamba hakiwafai watu wa aina nyingine.
Hivyo pale mtu ambaye humlengi anapokuambia labda ungefanya hivi au vile, hukimbilii kukubaliana naye na kuharibu kitu chako. Badala yake unamweleza wazi kwamba inalenga watu wa aina gani, wanaotaka matokeo gani.
Hilo halimaanishi kwamba hautapokea maoni ya kuboresha zaidi unachofanya.
Hayo utayapokea sana na kuendelea kuwa bora, lakini siyo kubadilika kila wakati ili kutaka kumridhisha kila mtu.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya au unachouza, chagua kabisa ni watu wa aina gani unaowalenga. Wasikilize hao na wape kipaumbele. Wale ambao huwalengi, ambao hawawezi kuendana na kitu kama kilivyo, wasikusukume ubadili kitu hicho ili uwapate. Kama hawawezi kuendana na kitu kama kilivyo, ni dhahiri hata ukikibadili hawataweza kuendana nacho.
Tafakari;
Kadiri unavyokazana kufanya kitu kimfae kila mtu, ndivyo unavyoishia kuwa na kitu ambacho hakimfai yeyote.
Kupata walio sahihi kwenye kitu chochote kile lazima uwe tayari kukosa wasio sahihi.
Kocha.