Rafiki yangu mpendwa,

Kuna kauli hizi muhimu na zenye nguvu sana kuhusu tabia;

  1. Huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga.
  2. Asilimia 60 ya mambo tunayofanya kila siku ni kwa tabia.
  3. Kujenga tabia ni kugumu, kuvunja tabia ni kugumu zaidi.
  4. Kujenga tabia ni sawa na kumfunga mtu kwa uzi, mzunguko mmoja hauna nguvu, ila unaporudiwa rudiwa unakuwa na nguvu ambayo haiwezi kuvunjwa kirahisi.
  5. Tabia zetu ndizo zinazoamua hatima yetu.

Rafiki, kwa kauli hizo kuhusu tabia, unajionea wewe mwenyewe jinsi unavyopaswa kuwa makini kwenye tabia. Kwani tabia ndiyo zenye nguvu ya kukujenga au kukubomoa.

Ni kwa kuzingatia hilo KISIMA CHA MAARIFA kimekuwa kinaandaa CHANGAMOTO YA SIKU 100, ambapo unachagua kitu kimoja tu ambacho utakifanya kila siku bila ya kuacha kwa siku 100.

Kwenye changamoto hii, unakuwa kwenye kundi ambalo kila siku unaweka ushahidi kwamba umefanya kile ulichochagua.

Ukiweza kufanya kitu kwa siku 100 bila kuacha, au ukaweza kufanya kwa siku nyingi zaidi, kitu hicho kinakuwa tabia kwako, inakuwa rahisi kwako kuendelea kukifanya kila siku.

Napenda kuchukua nafasi hii kukukaribisha ushiriki CHANGAMOTO YA SIKU 100 ambayo itaanza siku ya jumatatu ya tarehe 14/02/2022 na kumalizika jumapili ya tarehe 29/05/2022.

Hizi zinakuwa siku 100 za kufanya kitu bila kuacha na bila kutafuta sababu au kisingizio.

Ni siku 100 za kujenga msingi wa tabia utakayodumu nayo kwa muda mrefu, maana kama utaweza kufanya siku 100 bila kuacha, kitu hicho kitakuwa sehemu ya maisha yako.

Changamoto ya mwaka huu itafanyika kwenye kundi maalumu la Whatsapp ambapo unaweza kujiunga kwa kufungua kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/G91eD4TykPT8PjM1wyNukX

SHERIA TATU KUU ZA CHANGAMOTO HII.

Ili siku hizi 100 ziweze kwenda vizuri na kuwa na manufaa kwa kila anayeshiriki, kuna sheria kuu tatu ambazo kila mshiriki anapaswa kuzizingatia.

Sheria ya kwanza ni kuonyesha matokeo (show results) na siyo sababu au visingizio.

Sheria ya pili ni kutokuvunja mnyororo (don’t break the chain), ukishaanza kufanya, endelea bila kuvunja mnyororo huo wa ufanyaji.

Sheria ya tatu ni kutokukosa mara mbili (never miss twice), maisha yana changamoto na vikwazo vya hapa na pale. Kuna siku unaweza kubanwa kweli kweli na ikatokea umeshindwa kufanya au kuonyesha ushahidi. Ikitokea hivyo mara moja, kesho yake rudi kwenye kufanya, hupaswi kuruhusu itokee mara mbili kwa mfululizo.

Rafiki, hizo ndizo sheria tatu muhimu za changamoto hii, na pale zinapokushinda, utapaswa kuyaaga mashindano wewe mwenyewe bila ya kusubiri kuondolewa.

VITU UNAVYOWEZA KUFANYA KWENYE CHANGAMOTO HII.

Chochote unachotaka kukijenga kuwa tabia kwenye maisha yako ili uweze kufanikiwa, unaweza kukifanya kwenye CHANGAMOTO hii ya siku 100.

Muhimu ni kitu hiki kiweze kupimika katika kufanya na uweze kuonyesha ushahidi kwamba kweli umefanya.

Katika changamoto za nyuma watu wameweza kufanya yafuatayo;

  1. Kusoma kitabu kila siku bila kuacha na kuonyesha ushahidi wa kuandika kwa ufupi kitabu ambacho mtu amesoma na kile alichojifunza kwenye siku hiyo.
  2. Kuandika kila siku ambapo mtu anaonyesha sehemu ya maandiko aliyofanya na idadi ya maneno aliyoandika kwenye siku. Kama ni kuandika kwenye blog mtu anaweka makala aliyopost kila siku.
  3. Kufanya mazoezi kila siku ambapo mtu anatuma picha akiwa anafanya mazoezi kila siku.
  4. Kuweka akiba kila siku ambapo mtu anatuma risiti ya akiba aliyoweka au ujumbe wa malipo aliyoweka kwenye akaunti maalumu ya akiba.
  5. Kufanya kazi za kibunifu kila siku ambapo mtu anashirikisha picha au mfano wa kazi ya kibunifu aliyofanya.
  6. Kufanya masoko ya biashara kila siku ambapo mtu anaonyesha ushahidi wa juhudi za masoko alizofanya kila siku kama kutembelea watu, kupiga simu au kutuma ujumbe wa simu au email.
  7. Kuamka asubuhi na mapema kila siku ambapo mtu anatuma ushahidi muda ambao ameamka na kila baada ya nusu saa kwa masaa mawili ya kwanza anaeleza nini anafanya.
  8. Kuipangilia siku kwa kuorodhesha mambo ya kufanya na kujifanyia tathmini mwisho wa siku.
  9. Kuyaandika malengo makubwa mara tatu kwa siku na kushirikisha mara hizo tatu.
  10. Kujifunza lugha mpya kila siku kwa kutuma ushahidi wa uliyojifunza na mazoezi mbalimbali unayofanyia kazi.
  11. Kuacha kutumia mitandao yote ya kijamii na kutumia muda huo kwa mambo yenye tija.
  12. Kufikiria mawazo mapya 10 kila siku ya kuongeza kipato au kupiga hatua zaidi na kuyashirikisha.
  13. Kuacha matumizi ya vilevi na vyakula visivyo vya afya.
  14. Kufanya matembezi kila siku na kutumia app inayoonyesha hatua ambazo umetembea.
  15. Kujaribu kitu kipya kila siku na kuonyesha ushahidi wa kile ulichojaribu.

Rafiki hayo ni baadhi ya mawazo tu, lakini chochote unachotaka kufanya, unachoweza kukipima na kuonyesha ushahidi unaweza kukifanya kwenye CHANGAMOTO YA SIKU 100 na ukaweza kupiga hatua kubwa.

MASWALI NA MAJIBU.

Hapa kuna majibu ya maswali ambayo yamekuwa yanaulizwa sana kuhusu changamoto hii.

Swali; changamoto inafanyika wapi?

Jibu; changamoto inafanyika kwenye kundi maalumu la whatsapp ambapo unajiunga na kutuma ushahidi wako kila siku kwamba umefanya. Kujiunga na kundi fungua link hii; https://chat.whatsapp.com/G91eD4TykPT8PjM1wyNukX

Swali; vipi kama nataka kufanya kitu ambacho siwezi kupima au kutuma ushahidi?

Jibu; hakuna kitu cha aina hiyo, wasiliana na Kocha kwenye hicho unachopanga kufanya na atakuonyesha njia bora ya kupima na kutuma ushahidi.

Swali; vipi kama nitakosa mtandao na kushindwa kuonyesha ushahidi japokuwa nimefanya?

Jibu; sheria za changamoto zipo wazi, usikose mara mbili. Na kama unaweza kuja kuonyesha ushahidi wa siku ambazo hukuweza kutuma, unaweza kuendelea na changamoto.

Swali; vipi kama ninachotaka kufanya sipo tayari kuonyesha kwa watu wengine?

Jibu; kuna programu mbalimbali za ukocha ambazo zinaweza kukusaidia kwenye hilo, ambapo utasimamiwa na Kocha moja kwa moja katika kufanya kila siku. Wasiliana na Kocha kwa ajili ya programu hizo.

Swali; nataka kuandika kwenye blog kila siku ila sina blog.

Jibu; wasiliana na Kocha na atakuandalia blog unayoweza kuandika moja kwa moja hata kwa kutumia simu yako.

Swali; nataka kuandika kitabu lakini sijui ni muundo gani wa kufuata.

Jibu; wasiliana na Kocha na atakupa maelekezo ya namna ya kukamilisha hilo.

Swali; nataka kusoma vitabu ila sijui nisome vitabu gani.

Jibu; wasiliana na Kocha na atakushauri vitabu vizuri vya kusoma.

Swali; napata msukumo wa kushiriki changamoto hii lakini sijui nifanye nini.

Jibu; wasiliana na Kocha na upate mazungumzo naye, utajua kipi cha kufanya.

Swali; kuna zawadi yoyote kwa anayekamilisha changamoto ya siku 100?

Jibu; ndiyo, zawadi zipo, zitatangazwa na Kocha kwa wale watakaokuwa wamekidhi vigezo.

Karibu sana kwenye mchaka mchaka wa siku 100 za kufanya bila kuacha ili uweze kujijengea tabia utakayodumu nayo kwa maisha yako yote.

Kujiunga na kundi maalumu la kushiriki changamoto hii, fungua kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/G91eD4TykPT8PjM1wyNukX

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Muuza Matumaini Kocha Dr. Makirita Amani.

www.amkamtanzania.com

0717396253