2598; Ni tofauti kwa kila mtu.
Umewahi kufundishwa kitu fulani,
Au kusoma kitu fulani,
Au kusikia ushuhuda wa mtu fulani.
Halafu ukajiambia, hayo yanawezekana kwa watu wengine ila siyo kwangu.
Hali yangu ni tofauti, halafu unajiridhisha kwa kuorodhesha yale ambayo unaamini kwako ni tofauti.
Labda huna kipato kabisa,
Au umetoka familia masikini sana,
Au una madeni makubwa,
Au huna elimu kubwa,
Au umejaribu mara nyingi na kushindwa.
Na mengine mengi unayoweza kujiambia.
Sababu hizo zitakuwa sahihi kabisa kwako na zitakuridhisha kabisa.
Lakini huko ni kujidanganya tu.
Kwani hata wale uliowaona wamepiga hatua, siyo kwamba kila kitu kilikuwa sawa kwao.
Hata wao hali zao zilikuwa tofauti pia.
Na wengine wakiwa na hali mbaya kuliko hata wao.
Umewahi kwenda hospitali ukiwa unaumwa, halafu ukaona wengine wanaoumwa hasa na ukajiambia wewe huumwi?
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio.
Unaweza kujiona una hali ngumu, lakini kuna waliokuwa na hali ngumu kuliko wewe na wameweza kupiga hatua.
Maarifa mengi ni ya jumla,
Ushauri mwingi ni wa jumla,
Hali za kila mtu ni tofauti na za kipekee.
Usisubiri mpaka upate maarifa na ushauri wa kipekee kwako.
Tumia maarifa na ushauri uliopo kwa kuugeuza kuwa wa kipekee kwako na uweze kufanya makubwa.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapojifunza kitu na ukajiambia hiki halitanifaa mimi kwa sababu nipo tofauti, jikamate hapo hapo na jiulize ni namna gani utakitumia kwenye hiyo hiyo hali uliyonayo.
Usijiridhishe na hali yako, bali pambana kuwa bora zaidi.
Tafakari;
Kusubiri mpaka upate kitu kinachoendana na wewe moja kwa moja ni kujichelewesha. Kila mtu yuko tofauti, tumia huo huo utofauti wako kufanya makubwa.
Kocha.