2599; Mafanikio ni usumbufu.
Unaweza kushtuka kidogo hapo, iweje mafanikio ni usumbufu wakati ndiyo kitu tunachofundishana hapa kila siku?
Na nikuambie tu, hicho ni kitu ambacho wengi huwa hawakijui mpaka pale wanapofanikiwa.
Na kutokujua hilo, huwa ndiyo chanzo cha anguko lao.
Mafanikio huwa yanavuta kwako fursa zaidi na pia usumbufu zaidi.
Usipojua hili na kuwa makini, mafanikio yataleta anguko kubwa kwako.
Iko hivi, unapokuwa unaanzia chini kabisa, hakuna anayehangaika na wewe. Upo chini, watu hawaoni namna wanaweza kunufaika na wewe, hivyo hawakusumbui.
Utakuwa na muda wako wa kuweka juhudi zako zote kwenye kile unachofanya.
Kwa kufanya hivyo kwa muda mrefu utaanza kufanikiwa, utatoka chini na kwenda juu zaidi.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyopata fursa nzuri zaidi za kufanikiwa.
Halafu sasa usumbufu unaanza kuja. Watu wanaona umefanikiwa, wanaona kuna namna wanaweza kunufaika kupitia wewe.
Hapo ndipo watu watakuja kwako wakitaka misaada ya aina mbalimbali.
Taasisi na vikundi mbalimbali vitataka uwe mwanachama wao na kukupa nafasi ya uongozi.
Vyombo vya habari navyo vitataka kukuhoji na utoe historia yako kwa wengine.
Utapewa mialiko ya kuwa mzungumzaji kwenye mikutano na makongamano mbalimbali.
Serikali na mamlaka zake nayo haitakuwa mbali kuhakikisha unalipa kila kodi na tozo unayopaswa kulipa.
Halafu sasa kuna wale wambeya ambao watakuwa wanazusha mambo mbalimbali kuhusu wewe, ili tu wapate umaarufu fulani kupitia wewe.
Makosa mbalimbali uliyofanya wakati uko chini yanaweza kufukuliwa pale unapofanikiwa na yakatumika kukuumiza kwa namna fulani.
Rafiki, sikuelezi haya ili kukutisha au kukushawishi usifanikiwe.
Pambania mafanikio yako sana, ila jiandae na usumbufu utakaokuja na mafanikio hayo.
Bila maandalizi sahihi, utaishia kwenye anguko baya.
Hatua ya kuchukua;
Kadiri unavyopiga hatua za mafanikio, endelea kujikinga na kila usumbufu unaokujia au utakaokujia.
Hakikisha kipaumbele chako cha kwanza kinabaki kwenye kile unachofanya, iwe umefanikiwa au la. Hiyo ndiyo njia ya kupata na kudumu kwenye mafanikio.
Tafakari;
Kabla hujafanikiwa unaweza kuwaona waliofanikiwa wana roho mbaya kwa sababu hawajakupa kitu fulani ulichotaka. Unapofanikiwa ndiyo unagundua huwezi kumpa kila mtu kila anachotaka na pia huwezi kuzuia watu wasikuone una roho mbaya.
Kocha.