2600; Ni bora ujue mapema.

Kama kitu hakitafanya kazi au hakitakufaa, ni bora ujue mapema kuliko uendelee kupoteza muda.

Kama kitu hakiwezi kuhimili msongo mkubwa ambao kinaweza kukutana nao, ni bora ujue mapema kabla ya msongo huo.

Hivyo mara zote jua ukweli na kuwa mkweli na kijaribu kila kitu kwa viwango vya msongo ambao unaweza kutokea.

Kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa wanakwenda kinyume na hilo na ndiyo maana mambo yao yanakuwa magumu na kushindwa kufanikiwa.

Kama inabidi udanganye au uigize ndiyo uweze kujenga na kuendeleza mahusiano na mtu mwingine, iwe ni ya urafiki, ndoa, biashara na mengineyo, jua hapo hakuna mahusiano.
Uongo na maigizo vina mwisho na huo ndiyo utakuwa mwisho wa mahusiano yenyewe.

Kama mahusiano hayawezi kudumu bila uongo na maigizo ni bora kujua mapema na yakavunjika kuliko kuweka nguvu na muda wako na baadaye yaje yavunjike.

Kadhalika watu wamekuwa wanabembeleza sana vitu, wanaona wakivipa msongo mkubwa wataviharibu au kuvipoteza.
Ni mpaka pale asili inapokuja kuvipa kitu hicho msongo mkubwa na kukisambaratisha kabisa.

Miti inayoota jangwani au eneo lenye upepo huwa imara kuliko miti inayoota eneo lenye maji mengi na utulivu.
Hali ya hewa ikibadilika, ni miti iliyoota pazuri ndiyo itaathirika zaidi.

Chochote unachojenga, kama unataka kidumu hakikisha kinaweza kuhimili msongo wa kila aina. Kinaweza kuvuka magumu mbalimbali na kusimama imara.

Kuna wakati unaweza kupenda sana kitu kiasi cha kudanganya ili ukipate na kukilinda kwa kila namna ili usikipoteze.
Huko ni kujidanganya na kujipotezea muda.
Kama kitu hakiwezi kuhimili ukweli na msongo ni kitu ambacho hakiwezi kudumu kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua;
Usikubali kupoteza nguvu na muda wako kwenye kitu ambacho hakiwezi kuhimili kanuni za asili.
Mara zote simama kwenye ukweli, kama kitu kitashindikana kwa sababu ya kweli, basi hakiwezekani.
Hata kama utakipata kwa uongo ni kwa muda tu, ukweli utakuwa wazi na utakikosa.

Tafakari;
Kanuni za asili haziwezi kuvunjwa wala kupindishwa. Usijidanganye kwa muda kwa kwenye kinyume na kanuni za asili. Chochote ambacho hakiwezi kuhimili ukweli na msongo, hakiwezi kudumu. Jua hili na ulisimamie mara zote.

Kocha.