#SheriaYaLeo (105/366); Ione dunia kama hekalu lililoungana.

Dunia ni hatari na maadui wako kila mahali.
Siyo kila mtu anakutakia mema.
Na kadiri unavyopambana kufanikiwa, ndivyo unavyotengeneza maadui wengi zaidi.

Hilo linaweza kukufanya ujitenge na watu na kuamua kufanya mambo yako kivyako.
Utadhani kufanya hivyo kunawanyima maadui zako fursa ya kukudhuru.
Lakini hilo ni hatari kubwa zaidi.

Kadiri unavyojitenga na watu ndivyo unavyojiweka kwenye hatari ya kudhurika zaidi.
Maana wataunda njama na siri mbalimbali za kukudhuru ambazo hutaweza kuzijua.

Ichukulie dunia kama hekalu kubwa ambalo vyumba vyake vimeungana.
Kujifungia kwenye chumba kimoja ni kujikosesha mengi mazuri.
Badala yake ingia na kutoka kwenye vyumba mbalimbali.

Jichanganye na watu na jua yale yanayoendelea.
Kwa njia hiyo hakuna njama au siri zitakazotengenezwa juu yako na usizijue.

Kadiri unavyojichanganya na wengi na kujua yale yanayoendelea ndivyo unavyopunguza nguvu ya maadui zako kukudhuru.

Mafanikio na mamlaka ni vitu vinavyopata nguvu kutoka kwa watu.
Kadiri unavyoweza kujichanganya na wengi ndivyo unavyopata nguvu zaidi.

Muhimu pia usitabirike, maana mnyama anayetabirika ni rahisi kuwindwa kuliko asiyetabirika.

Sheria ya leo; Kupata nguvu, mamlaka na mafanikio, jiweke katikati ya vitu. Jichanganye na watu wa aina mbalimbali na tengeneza washirika wa kila aina ili maadui zako wasipate nguvu ya kukudhuru.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji