2607; Kama siyo maamuzi ya kufa na kupona.

Kuna maamuzi ya kufa na kupona, maamuzi ambayo ukikosea yana madhara makubwa na huwezi kuyabadili tena.

Hayo ni maamuzi machache sana kwenye maisha na utakutana nayo mara chache mno katika kipindi chote cha maisha yako.

Lakini kwenye maisha ya kila siku, maamuzi mengi unayofanya siyo ya kufa na kupona. Ni maamuzi ambayo hata ukikosea hayana madhara yoyote na unaweza kuyabadili.

Inashangaza jinsi watu wanavyopoteza muda mwingi katika kufanya maamuzi hayo ambayo siyo ya kufa na kupona.

Wewe usikubali kuwa hivyo.
Unapojikuta njia panda na hujui ni maamuzi gani ufanye, kama siyo ya kufa na kupona basi chagua chochote.

Kuliko upoteze muda kusubiri, chagua chochote na uanze kufanyia kazi.
Kama utakuwa umekosea basi utabadili.
Na uzuri ni utajifunza mengi kupitia maamuzi hayo hata kama unakuwa umekosea.

Chukua mfano unajiuliza ni biashara gani ufanye.
Haya siyo maamuzi ya kufa na kupona.
Hivyo badala ya kusubiri mpaka ujue kwa hakika ni biashara gani sahihi kwako, wewe anza na biashara yoyote.
Chagua kuuza chochote ambacho watu wana uhitaji nacho.
Hata kama haitakuwa biashara sahihi kwako, kuna mengi sana utakayojifunza na baadaye kuweza kwenda kwenye biashara sahihi kwako.

Hatua ya kuchukua;
Kwa maamuzi yoyote yasiyo ya kufa na kupona usipoteze muda wowote katika kuyafanya. Chagua chochote na fanyia kazi, ukigundua hayakuwa maamuzi sahihi yabadili na kufanya yaliyo sahihi.
Hivyo ndivyo unavyoweza kupiga hatua haraka na kuwaacha wengine wakiwa wanashangaa.

Tafakari;
Muda mwingi unapotezwa kusubiri maamuzi sahihi wakati maamuzi yoyote hayana madhara makubwa. Muda unaopoteza kwa kutokufanya maamuzi unaupoteza bila kujifunza chochote. Ni bora ufanye maamuzi yoyote, hata kama umekosea, kuna mengi utakayojifunza.

Kocha.