2622; Sababu zipo tayari.

Kama unataka kufanya kitu, au hutaki kukifanya, sababu zipo tayari.

Kama utafanikiwa au utashindwa, sababu zipo tayari.

Yaani sababu tayari ziko mbele yako, ni wewe tu uchague unataka nini, halafu uchukue sababu zinazoendana na kile unachotaka.

Kama unataka kweli kupata kitu, sababu za kukitaka tayari unazo.
Na kama hukitaki kweli kitu, sababu za kutokukitaka tayari unazo.

Sababu ni rahisi kama chumvi, ndiyo maana watu wote makini huwa hawasikilizi sababu.
Wao wanachoangalia ni matokeo, wakijua hicho ndicho mtu alikitaka kweli.

Sababu zinaweza kuridhisha na kufariji, lakini hazibadili chochote kile.
Hatua unazochukua na matokeo unayopata ndiyo vinavyoleta mabadiliko.

Hatua ya kuchukua;
Usipoteze muda wako kwenye sababu, fanya au usifanye, ila usijidanganye na sababu. Kama kweli unakitaka kitu utakipata na kama hukitaki hutakipata.
Usiendekeze sababu za wengine, angalia wanachofanya, hicho ndiyo wamedhamiria kweli, sababu ni kujidanganya na kujifariji tu.

Tafakari;
Unaweza kutoa sababu au unaweza kutoa matokeo. Huwezi kutoa vyote kwa pamoja.
Hivyo chagua vyema kabisa unaamua kutoa nini, halafu usilalamike pale unaopata kile kinachoendana na ulichochagua.

Kocha.