#SheriaYaLeo (134/366); Watambue wenye majigambo kabla hawajakunasa.

Watu wenye majigambo yaliyopitiliza (Narcissists) ni watu ambao ndani yao hawajiamini.
Wanatumia majigambo hayo kuficha udhaifu huo mkubwa ulio ndani yao.

Watu hao huwa wanajiona wao ni muhimu kuliko watu wengine na hivyo hutaka watu wote wawatii wao.
Huwa wanataka kila mtu awe kama wao na walio tofauti basi hawafai.

Wanapokuwa na wengine mara zote wanataka kuongelea kuhusu wao na kusifiwa.
Huwa hawapendi kukosolewa kwa namna yoyote ile, hivyo huwa wakali na kujitetea pale wanapokosolewa.

Ni watu wa kupata hasira haraka na kutaharuki pale mambo yanapokwenda tofauti na walivyopanga.
Wana maadui kila kona na yeyote asiyekubaliana nao basi ni adui kwao.
Huwa wanapenda kuonyesha kwamba wameonewa na hawana hatia.

Wanatumia kila njia kupata huruma ya wengine.
Lakini ndani ni watu wenye nia ya kutawala wengine na kuwatumia kwa manufaa yao wenyewe.

Ni watu wenye wivu sana pale wanapoona mtu mwingine anapata umaarufu kuliko wao.
Hufanya kila namna ili kuhakikisha wanaongelewa zaidi kuliko wengine.
Wapo tayari hata kuvuruga mambo ya wengine ili tu waongelewe.

Ni watu ambao hawapo vizuri kwenye kujenga mahusiano na kuyadumisha.
Kwao watu ni vitu vya kutumia, hivyo kama hawana namna ya kumtumia mtu hawahangaiki naye.
Na pia mahusiano yao huwa yahadumu kwa sababu kosa dogo huwa wanalikuza sana kutokana na kutokujiamini kwao.

Ni muhimu sana uwajue watu hawa kwa tabia zao na kuwaepuka mapema.
Kwani ukishaingia kwenye anga zao huwa ni vigumu sana kujinasua, watakusumbua kwa muda mrefu.

Sheria ya leo; Watu wenye majigambo huwa wanataka kila kitu kiwe chini yao. Hawawezi kuvumilia pale wanapoona au kuhisi kuna mtu mwingine yuko juu yao kwa namna yoyote ile. Waepuke sana watu wa aina hiyo kwa sababu wakiona au kuhisi uko juu yao watakusumbua sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji