2633; Kafanyaje huyu?

Kuna picha ya kichekesho (meme) inayozunguka sana kwenye mitandao.

Kwenye picha hiyo mtu anayeonekana kuzimia amebebwa kwenye machela na watu wawili.

Mmoja anauliza mtu huyo aliyebebwa amefanya nini?
Mwingine anajibu kitu alichofanya mtu huyo na kupata matokeo ambayo hakutegemea.

Watu na taasisi mbalimbali wamebadili maelezo ya mtu wa pili kuendana na kile wanachofanya wao.
Wanafanya hivyo kuwashawishi watu kuchukua hatua sahihi ili nao wasijikute kwenye hali ya kuzimia na kubebwa kwenye machela.

Unaweza kupuuza picha hiyo na kuona ni kitu tu cha utani, lakini kusambaa kwake kwa kasi kuna funzo kubwa sana.

Kwanza ni kuhusu masoko, kitu kinachosambaa kwa kasi kwa sababu kinaendana na watu huwa ni kizuri sana kwenye masoko.
Masoko hayapaswi kuwa kitu kipya kabisa, bali kitu kinachoendana na asili ya watu.

Pili ni kupenda mteremko, watu huwa hawapendi kuukiza kichwa kuja na kitu cha tofauti. Bali huenda na kile ambacho tayari ni maarufu.

Tatu ni mategemeo kwenye chochote ambacho unafanya. Unapojiwekea mategemeo ya juu na yasifikiwe, unaishia kuumia sana.
Hivyo ni vyema kwa kila unachofanya, ujipe nafasi ya kupata matokeo ya tofauti na unavyotegemea.

Jifunze kutoka kwenye kila kitu hata kama kinaonekana ni kidogo na cha hovyo kiasi gani.

Hatua ya kuchukua;
Unapoona kitu kidogo kinasambaa kwa kasi sana, jifunze ndani yake.
Usikipuuze na kuona hakina maana, jua jinsi ambavyo kimegusa asili ya watu na jifunze jinsi ya kufanya hivyo kwa vitu unavyofanya pia.

Tafakari;
Kitu kusambaa kwa kasi sana ni kiashiria kwamba kimegusa sehemu muhimu kwa watu.
Japo inaweza kutokea kama ajali tu, bado kuna mengi ya kujifunza kwenye hali za aina hiyo.

Kocha.