#SheriaYaLeo (154/366); Tumia uhaba kuongeza thamani.
Ni kanuni ya msingi kabisa ya uchumi kwamba kitu kinapopatikana kwa wingi, thamani yake inapungua na hivyo bei yake kuwa chini.
Lakini kitu kinapopatikana kwa uhaba, thamani yake inakuwa kubwa na bei yake kuwa juu.
Ili kuongeza thamani yako binafsi na ya kile unachofanya, tumia kanuni hii ya uhaba.
Kwako binafsi usiwe mtu wa kuonekana au kupatikana kirahisi.
Maana kadiri watu wanavyokuona na kukupata kirahisi, ndivyo wanavyokuchukulia kawaida na hivyo thamani yako kuwa chini.
Lakini kama huonekani na hupatikani kirahisi, watu wanakuthamini sana.
Kadhalika kwa kile unachofanya, kama kinapatikana kwa urahisi au kinaweza kufanywa na kila mtu thamani yake inakuwa chini.
Fanya kitu cha kipekee ambacho watu hawawezi kukipata sehemu nyingine isopokuwa kwako tu.
Hapo watu watakithamini sana na unaweza kukipa gharama kubwa na bado watu wakawa tayari kukilipia.
Kama watu hawakuthamini wewe au kile unachofanya, jibu unalijua, ni kwa sababu upatikanaji umekuwa rahisi.
Hivyo hatua ya kuchukua ni kama wafanyabiashara wanavyojua, kuiondoa bidhaa sokoni kwa muda ili kuipandisha bei.
Watu wanapokukosa au kile unachofanya kinapokuwa chs kipekee ambacho hawawezi kupata pengine, thamani inakuwa kubwa.
Kwa zama za sasa ambapo kupatikana kwa watu kumekuwa rahisi sana na kila mtu anafanya kile ambacho wengine wanafanya, sheria hii ni muhimu sana ili kufanikiwa.
Huwezi kufanikiwa kama unapatikana kirahisi na kama unafanya kile ambacho wengine pia wanafanya.
Weka uhaba kwako binafsi na kwenye kile unachofanya na thamani yako itakuwa kubwa.
Sheria ya leo; Kadiri unavyoonekana na kufikika kirahisi ndivyo watu wanavyokuchukulia kawaida na thamani yako kuwa ndogo. Kama umeshazoeleka sana kwa watu chagua kupotea kwa muda na kufanya vigumu watu kukupata. Hilo litawafanya watu waanze kukuongelea na kutaka zaidi kukupata, kitu kitakachopandisha thamani yako.
Kadhalika pia kwa kile unachofanya, hakikisha watu hawawezi kukipata pengine isipokuwa kwako tu.
Tengeneza thamani kwa kutumia uhaba.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
Ahsante Sana kocha.
LikeLike
Karibu
LikeLike