2651; Lile wazo limepotea.
Hizi kurasa huwa naandika kutokana na yale ninayokutana nayo kila siku.
Kuanzia kujifunza, kukochi wengine na mawazo yanayonijia kulingana na mambo ninayokutana nayo.
Jana wakati niko safarini kuna wazo la kuandika lilinijia, nikawa nimelifikiria vyema kwa namna ya kuliandika.
Lakini kutokana na uchovu sikuandika wazo hilo mahali, nilijiambia hili ni la kawaida kabisa, siwezi kulisahau.
Cha kushangaza, leo najaribu kukumbuka wazo hilo lakini nimeshindwa kabisa.
Kila njia ninayojaribu kuvuta kumbukumbu za wazo hilo inaleta mawazo mengine lakini siyo lile nililodhamiria.
Kwa kawaida huwa nina utaratibu wa kuandika kila wazo linalonijia, ila kwa uchovu niliokuwa nao niliruhusu uvivu kuzuia hilo.
Najua nitakuja kukumbuka wazo hilo siku nyingine, lakini itakuwa imeathiri mpango wangu.
Hatua ya kuchukua;
Usiamini kumbukumbu zako, kwa kila wazo zuri unalolipata, liandike mahali mara moja moja kabla hujalisahau.
Usijidanganye kwamba utakumbuka, wakati wa kukumbuka unapofika, ndiyo utagundua kwamba kumbukumbu zako zinaweza kukusaliti.
Tafakari;
Akili zetu huwa zinapokea mawazo mengi sana kila wakati.
Mawazo yanayobaki kwenye kumbukumbu zetu ni yale tunayoyapa uzito zaidi.
Na njia ya kwanza kwenye kuyapa mawazo uzito ni kuyaandika mahali.
Kocha.