2654; Kumbuka wewe ni binadamu.

Kadiri ninavyokaa kwenye hii huduma ya ukocha, ndivyo ninavyojifunza kwa karibu tabia za watu na kuwa bora zaidi katika kuwasaidia kufika kule wanakotaja kufika.

Zamani alikuwa akija mtu kwangu, mwenye njaa kweli ya mafanikio na anayesema yupo tayari kufanya kazi usiku na mchana ili kupata anachotaka nilikuwa naona nimepata mtu sahihi.
Hivyo nampa moyo apambane kweli kweli na kumsimamia kwa karibu.

Lakini huwa haipiti muda mrefu mtu wa aina hiyo huishia kuchemka na tena anachemka vibaya sana kiasi cha kupotea kabisa.

Nilichojifunza ni mwanzo watu wanakuwa na hamasa kubwa ambayo inakuwa na nguvu ya kuuburuza mwili kwa vile mtu anataka.
Lakini haichukui muda mwili unamsaliti mtu, unakuwa hauwezi tena kuburuzwa, hata kama mtu ana hamasa kiasi gani.

Inafika mahali mwili umechoka kweli kweli na hakuna namna nyingine.
Na hapo ndipo mtu anachemka na kushindwa kabisa kuendelea.

Sasa nimeboresha, pale ninapokutana na watu wa aina hii, huwa nawashauri waende kwa kasi ambayo itaupa mwili nafasi ya kupumzika.
Mwili upate sehemu yake ya mapumziko ili uweze kujenga nguvu ya kuendelea na safari.
Bila ya mapumziko ya aina hiyo, lazima mtu ataishia kuchemka.

Mashine zenywe ambazo hazina hisia bado zina kiasi cha kufanya kazi na kupumzika, sembuse binadamu mwenye hisia zake?

Unaweza kuwa na hamasa kubwa sana, lakini usisahau wewe ni binadamu. Ukiusukuma huo mwili kupitiliza, utaishia kukusaliti.

Huwa nakumbuka sana hadithi moja ya mtu aliyeenda kwa mtawa wa kibudha akamuuliza anataka kufikia utambuzi wa hali ya juu, anapaswa kufanya tahajudi kwa miaka mingapi? Mtawa huyo akamjibu miaka 10.
Mtu huyo akamuuliza tena, vipi kama nikifanya usiku na mchana, itanichukua miaka mingapi? Mtawa akamjibu miaka 20.
Unaweza kuona hapo, kadiri mtu anavyoweka juhudi za kupitiliza, ndivyo muda unakuwa mrefu zaidi, maana huko katikati kuna vipindi atasimama muda mrefu kutokana na uchovu wa kupitiliza.

Hatua ya kuchukua;
Jikumbushe namba zetu za 16/6/50.
Masaa yasiyozidi 16 ya kufanya kazi kwa siku. Masaa nane yanayobaki kwa sehemu kubwa yawe ya kupumzika.
Siku 6 za kufanya kazi kwa wiki. Siku moja ya wiki iwe ya mapumziko makubwa kwako.
Wili 50 za kufanya kazi kwa mwaka. Wiki mbili zinazobaki ziwe za mapumziko makubwa kwako.
Unaweza kuona unapoteza muda, lakini kinachokwenda kutokea unatumia kwa ufanisi zaidi muda unaokuwa nao.

Tafakari;
Kwa kuweka juhudi kupitiliza, unaishia kupunguza uzalishaji na ufanisi wako.
Wewe ni binadamu, mwenye mwili ambao unachoka.
Mapumziko ni sehemu muhimu katika juhudi kubwa unazoweka.
Tenga na linda sana muda wako wa mapunziko.

Kocha.