2660; Huwezi kuhangaika na kila kitu.
Kwenye kila tasnia, mabadiliko na matokeo makubwa huwa yanazalishwa na vijana.
Lakini cha kushangaza vijana hao hao wakishafikia mafanikio makubwa kwenye tasnia zao na kuwa watu wazima, wanaacha kufanya makubwa.
Hapa napenda tujifunze kitu kikubwa sana ambacho tunaweza kukitumia kwenye kila umri na kikatusaidia kufanya makubwa.
Mtu anapokuwa anaanza, hasa akiwa kijana, anakuwa hana mambo mengi.
Hakuna wengi wanaomjua na pia anakuwa hana wengi wanaomtegemea.
Hilo linamfanya aweke umakini mkubwa kwenye kile anachofanya.
Umakini huo ndiyo unaomsaidia kuweza kuzalisha matokeo makubwa.
Lakini sasa mtu huyu anapofanikiwa, anaanza kupata umaarufu, kila mtu anamjua.
Anapata maombi na mapendekezo mbalimbali nje ya kile anachofanya.
Anapata nafasi za uongozi na fursa nyingine nje ya kile anachofanya.
Matokeo yake ni hawezi tena kuweka juhudi kubwa kwenye kile alichokuwa anafanya na hilo linakuwa kikwazo kwake kuendelea kufanya makubwa.
Chukua mfano wa mwanasayansi anayechipukia, ambaye muda wake mwingi anauweka kwenye kufanya tafiti na kutoa machapisho mbalimbali.
Hilo linamfanya apande ngazi za juu.
Anapoonekana juu, anaanza kupewa fursa nyingine nje ya sayansi, labda anapewa nafasi ya uongozi au vitu vingine.
Hilo linampa majukumu mengine nje ya sayansi na hivyo kupunguza juhudi anazoweka kwenye sayansi.
Somo kubwa la kujifunza hapa ni hili, unapaswa kuweka umakini wako mkubwa kwenye kile unachofanya na kuachana na mengine yasiyohusika na hicho ulichochagua.
Kadiri unavyofanikiwa kuna fursa nyingi nje ya kile unachofanya zitakujia.
Zitakuwa fursa nzuri na zinazotamanisha, lakini jua zitakuwa kikwazo kwako kupiga hatua zaidi kwenye kile ulichochagua.
Lazima uwe tayari kuzikataa fursa nzuri, ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye lile eneo ulilochagua.
Chagua mambo machache ya kujihusisha nayo ili juhudi zako zisitawanyike na kukosa tija.
Lazima uwe tayari kukosa vitu vinavyoonekana vizuri kwa nje lakini ndani ni kikwazo kwako kufanya makubwa zaidi.
Hilo linahusisha pia mambo ya kijamii, ambayo ni mazuri kufanya, lakini ukiyaendekeza yanakuwa kikwazo kwako.
Tumekuwa tunajifunza sana kuhusu mwanga wa jua, ukitawanyika unaleta mwangaza, ukikusanywa unawasha moto.
Kadhalika kwa nguvu zako, ukizitawanya sana haziwi na madhara makubwa kama ukizikusanya sehemu moja.
Hatua ya kuchukua;
Kipi kipaumbele chako cha kwanza ambacho unaweka juhudi zako zote na kupuuza mengine?
Kwenye huu muongo wa kuelekea kwenye ubilionea biashara ndiyo kitu cha kwanza chako.
Jua wazi ni biashara ipi ndiyo itakuwa kipaumbele cha kwanza kwako kisha ipe nafasi kubwa na puuza mengine yasiyokuwa na tija kwenye hilo ulilochagua.
Tafakari;
Muda na nguvu ni rasilimali zenye uhaba na ukomo. Ukizitumia hovyo unakuwa umezipoteza na hazirudi tena.
Hivyo weka vipaumbele vyako sawa, na hakikisha unatumia rasimali hizo kwa yale muhimu tu, yasiyo muhimu yapuuze.
Huwezi kufanya kila kitu na huwezi kumridhisha kila mtu.
Chagua kwa usahihi.
Kocha.
Ahsante Sana kocha, kocha. Biashara ndio kila kitu kwangu kwa sasa.
LikeLike
Umechagua lililo sahihi,
Sasa pambana kwa kila namna.
Sema hapana kwa yote yasiyo na mchango kwenye hilo.
LikeLike
Safi sana,
Kaa humo.
LikeLike