2661; Wanakuvuruga usione uhalisia.
Mpishi mmoja mbobezi amewahi kusema njia ya haraka ya kujua kama chakula ni kizuri au kibaya ni kuangalia viungo ambavyo vimewekwa kwenye chakula hicho.
Akaendelea kusema unapoona chakula kina viungo vingi sana, jua siyo kizuri.
Hivyo wanaweka viungo vingi ili kukuvuruga usione uhalisia.
Alitumia maneno makali akisema; “wanakuwekea viungo vingi ili usigundue unakula chakula cha mbwa”.
Na hilo ni uhalisia kabisa, fikiria ulikuwa umetunza nyama au samaki kwa ajili ya kula, kisha ukagundua wameanza kuharibika na huna namna nyingine. Kinachofuata ni kuweka kila aina ya kiungo ili kupoteza ile ladha ya kuharibika.
Hilo ni kweli, siyo tu kwenye chakula, bali kwenye kila eneo la maisha.
Unapoona watu wanakazana kukipamba sana kitu, jua kina ubovu ndani yake.
Mapambo yanatumika kama njia ya kuwavuruga watu wasione uhalisia, ambao ni ubovu ilio ndani ya kitu hicho.
Na kwa kuwa huwa tunahadaika sana kwa macho, watu hutumia njia hii kutuvuruga ili tusichimbe na kuona ndani zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Pale unapokutana na kitu kinapambwa sana kwa nje, kataa kukiamini kwa haraka, badala yake jilazimishe kukichunguza kwa undani. Kwa mwanzo unaweza kuona siyo muhimu kufanya hivyo, ila unapozama ndani ndiyo unaona na kujua umuhimu wake.
Usikubali macho yako yaidanganye akili, bali tumia akili kuyafanya macho yauone uhalisia.
Tafakari;
Watu wanatumia nguvu nyingi kutengeneza mwonekano wa nje ambao ni tofauti kabisa na uhalisia wa ndani. Mara zote kuwa na mashaka na mwonekano wa nje, chimba zaidi kujua uhalisia wa ndani.
Kocha.
Shukurani Sana kocha. Kitu Kama kinapamba Sana kuna kitu kinafichwa. Huu ni ukweli mtupu.
LikeLike
Hakika
LikeLike
Nimelitafakari sana hili na nimejilidhisha ni ukweli usiopingika, lakini pia ni funzo la namna sahihi ya kumshawishi mteja
LikeLike
Karibu Frank
LikeLike