2662; Kama Ninge….

Hakuna njia rahisi ya kuyaharibu maisha yako na kujizuia kufanikiwa kama kuwa na majuto.

Kuangalia yale ambayo hukufanya au hukuchagua na kuona labda ndiyo yangekuwa bora ni uhakika unachofanya sasa hakiwezi kuwa bora.

Uliacha kazi na kuingia kwenye biashara, lakini mambo hayaendi kama ulivyotegemea.
Unaweza kujiambia, kama ningebaki kwenye kazi ningekuwa mbali zaidi.

Umeachana na biashara nyingi na kuchagua hiyo moja ambayo ndiyo unaweka juhudi zako zote, lakini bado mambo hayaendi vizuri.
Unaweza kujiambia kama ningechagua biashara nyingine mambo yangekuwa mazuri kwa sasa.

Uliwaacha wengine na kuoa au kuolewa na mtu uliyenaye sasa, lakini mahusiano yana misukosuko isiyoisha. Unaweza kujiambia kama ningeoa au kuolewa na mwingine maisha yangekuwa mazuri.

Hiyo ni mifano michache lakini unapata picha.
Kila mmoja wetu kuna wakati anatumia kauli hii ya kama ninge.
Hata kama uko kwenye foleni, unaweza kujiambia kama ningewahi zaidi, au kama ningetumia njia nyingine n.k.

Rafiki, leo nataka nikuambie hizo kama ninge hazina msaada wowote kwako.

Kwanza hujui kama ungechagua kingine matokeo yangekuwaje.
Unadhani yangekuwa mazuri, lakini ni vile hujafanya.
Ungefanya ungeujua uhalisia, kwamba hata huko siyo rahisi kama unavyofikiria.

Pili kufikiria yale ambayo hujafanya kunaondoa umakini wako kwenye kile unachopaswa kufanya sasa.
Pale unaposema kama ninge maana yake umeondoa umakini wako kwenye kile unachofanya sasa na kuupeleka kwenye kitu kingine.
Hilo litaathiri matokeo ya kile unachofanya.

Unapochagua kufanya kitu kimoja, kipokee kwa moyo wako wote na kubali hicho ndiyo bora kabisa kwa wewe kufanya.
Weka juhudi zako zote kwenye kufanya kitu hicho na sahau kuhusu vingine vyote.

Usijidanganye kwamba ungechagua kingine kingekuwa bora zaidi, hilo hujui.
Unachopaswa kujua ni kwamba ukiweka juhudi zako zote kwenye hicho ulichochagua, kitakuwa bora.

Hakuna juhudi zimewahi kuwekwa mahali na zisizae matunda.
Tatizo kwa wengi ni kuruhusu majuto kupunguza juhudi wanazoweka kwenye eneo walilochagua.

Hatua ya kuchukua;
Futa kabisa majuto kwenye maisha yako. Jifunze kwa kila unachopitia na kubali kile ulichochagua kwa asilimia 100. Kisha weka juhudi zako zote ili ukifanye kuwa bora kabisa.
Kila unapojikuta unajiambia kama ninge, jikamate hapo hapo na jiambie naenda kuweka juhudi kubwa zaidi kwenye hiki nilichochagua, maana ndiyo kilicho bora zaidi.

Tafakari;
Kuchagua ni jambo moja, kuwa na msimamo kwenye kile ulichochagua ni jambo jingine muhimu zaidi.
Pambana kuwa na msimamo, usiruhusu majuto kukuondoa kwenye kile ulichochagua.

Kocha.