2667; Sumu ya mafanikio.
Huwa kuna hadithi fupi kuhusu mwanzilishi wa Dubai ambayo huwa inazunguka sana mtandaoni.
Mwanzilishi huyo anaulizwa anauonaje mustakabali wa nchi yake, anajibu kama ifuatavyo;
Babu yangu aliendesha ngamia, baba yangu akaendesha ngamia, mimi ninaendesha Mercedea, mtoto wangu anaendesha Land Rover na mjukuu wangu atakuja kuendesha Land Rover. Lakini kitukuu changu kitakuja kuendesha ngamia.
Alipoulizwa kwa nini inakuwa hivyo akajibu;
Nyakati ngumu huwa zinatengeneza watu imara. Watu imara wanatengeneza nyakati rahisi. Nyakati rahisi zinatengeneza watu dhaifu. Na watu dhaifu wanatengeneza nyakati ngumu.
Akamalizi akisema;
Wengi hawataelewa hili, lakini unapaswa kutengeneza mashujaa na siyo wanyonyaji.
Hadithi hii ina funzo kubwa kwenye ngazi mbalimbali, kuanzia kwa mtu binafsi, taifa na hata dunia kwa ujumla.
Lakini leo tutaangalia kwa mtu binafsi.
Wengi wanapokuwa wanaanzia chini kabisa na hawana chochote, hupambana kwa kila namna.
Hufanya kazi usiku na mchana, huwa wajasiri na kushambulia kwa kila namna.
Juhudi hizo huwa zinawapa matokeo mazuri na kuanza kufanikiwa.
Na hapo ndipo shida huanzia, kwani mafanikio kidogo wanayoyapata huwa ni sumu kwa mafanikio makubwa zaidi.
Baada ya kupata mafanikio kidogo watu wanabadilika.
Hawajitumi tena kama awali.
Badala ya kushambulia wanaanza kulinda kile ambacho tayari wamekipata.
Badala ya kujituma kupitiliza wanaanza kujionea huruma na kujijali kupitiliza.
Wanajipa hadhi ambazo hawakuwa nazo.
Wanaacha fursa ambazo zingekuwa na manufaa kwao.
Hayo yote yanachangia anguko kubwa kwa watu hao baadaye.
Mafanikio yako madogo yanageuka kuwa sumu kwako mwenyewe.
Yanakuletea uvivu, mazoea na kujipa hadhi usiyokuwa nayo.
Mabadiliko hayo yanahamisha umakini wako na kujikuta ukihangaika na mambo yasiyo na tija kabisa kwako.
Kwa kuwa pia mafanikio unayokuwa umepata yanakupa vitu ambavyo awali hukuwa navyo, unajikuta ukivitumia kupita kiasi.
Ukomo uliokuwa nao mwanzo ambao ulikufanya uwe mbunifu na ujitume zaidi, unaondoka na hapo ndipo unapopoteza ubunifu na kuweka mazoea.
Hatua za kuchukua;
Kila siku kaa kwenye mtazamo wa siku ya kwanza, mtazamo wa huna ulichonacho hivyo unapaswa kupambana.
Haijalishi umefika wapi, mara zote taka kufika mbali zaidi ya hapo.
Usifanye kitu chochote kwa mazoea.
Usiwe mtu wa kulinda, bali mara zote shambulia.
Jiwekee ukomo utakaokusukuma kuwa mbunifu na kujituma zaidi.
Mfano hata kama una fedha za kukuwezesha kufanya chochote unachotaka, jiwekee ukomo kwenye kiasi unachoweza kutumia kwenye kila hali.
Tafakari;
Mafanikio ni mazuri, lakini yana hatari kubwa ya kumfanya mtu kuwa dhaifu kuliko alivyokuwa kabla ya kufanikiwa.
Unapaswa kuweka juhudi za dhati kuyazuia mafanikio yako yasiwe sumu kwako.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyopaswa kujiona bado hujafanikiwa ili upate nguvu ya kuendelea kuweka juhudi zaidi.
Kocha.
Asante kocha
LikeLike