2675; Haifanyi kazi…
Umejifunza njia za masoko za kuongeza wateja kwenye biashara yako.
Unatumia njia hizo, lakini bado wateja hawaongezeki.
Umejifunza njia ya kupunguza uzito wa mwili ni kula kwa afya na kufanya mazoezi.
Umefanya hivyo, lakini bado uzito haupungui.
Umejifunza njia ya kufika kwenye utajiri mkubwa ni kuweka akiba kwenye kila kipato chako, kisha kuwekeza akiba hiyo kwenye maeneo yanayokua thamani.
Umefanya hivyo, lakini bado hujapata utajiri.
Unachojiambia ni hiki; Hii kitu haifanyi kazi.
Na mimi sikukubalii wala sikukatalii.
Badala yake nina swali dogo kwako.
Je umefanya mara ngapi mpaka kufikia hitimisho hilo?
Isije kuwa umefanya mara chache tu halafu ndiyo ukafikia hilo hitimisho kama haifanyi kazi.
Kwani ili uweze kuona matokeo ya kitu chochote kile, lazima ukifanye kwa muda mrefu bila kuacha.
Unaikumbuka hadithi ya Thomas Edison, ya kufanya majaribio elfu 10 ndiyo kuweza kugundua taa ya umeme?
Hilo halijabadilika mpaka leo.
Hakuna chochote unachofanya mara moja au mara chache kikakupa matokeo unayoyataka.
Kila unachofanya, unahitaji kukifanya mara nyingi na kwa muda mrefu sana ndiyo kiweze kukupa matokeo unayoyataka.
Kinapaswa kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.
Usifanye kwa sababu unategemea matokeo ndiyo uendelee kufanya.
Fanya kwa sababu unapaswa kufanya, ndiyo sehemu ya mchakato wako na hutaacha kamwe.
Lakini hilo haimaanishi uendelee kufanya kwa mazoea, kwa namna ile ile huku ukitegemea matokeo tofauti.
Hata Edison hakufanya hivyo, hakurudia kitu kimoja mara elfu 10.
Bali alirudia kwa kuboresha na mwisho ndiyo akapata matokeo aliyoyataka.
Hatua ya kuchukua;
Fikiria ni vitu gani vipya umeshajaribu kufanya kwenye maisha yako ila ukawa unaishia njiani kwa sababu umeona havifanyi kazi.
Kila ulichoishia njiani umepoteza.
Ili kupata unachotaka, lazima ufanye unachopaswa kufanya kwa muda mrefu bila kuacha au kukata tamaa.
Je wewe huwa unafanya mara ngapi kabla hujajiambia haifanyi kazi?
Kuanzia sasa, ondoa hiyo kauli ya haifanyi kazi,
Badala yake nenda ukiboresha mpaka ifanye kazi.
Tafakari;
Umehangaika na mengi kwenye maisha yako lakini huna matokeo yoyote makubwa ya kuonyesha.
Hiyo ni kwa sababu hukai kwenye kitu kwa muda wa kutosha kuweza kuleta matokeo sahihi.
Badili hilo kama kweli unataka mafanikio makubwa.
Kocha.