2678; Huwezi kuboresha kisichokuwepo.
Watu wengi huwa wanakwama kuchukua hatua au kuahirisha kwa sababu wanasubiri ukamilifu.
Wanataka wafanye kitu ambacho kimekamilika kabisa na hakina madhaifu yoyote.
Lakini hilo ni kinyume na uhalisia.
Kompyuta ya kwanza kutengenezwa ilikuwa kubwa ya kujaza chumba kizima, huku uwezo wake wa kubeba kumbukumbu ukiwa mdogo.
Leo hii tuna kompyuta zinazoenea kwenye viganja vya mikono.
Kompyuta zimefika hapo kwa maboresho endelevu na siyo kusubiri ukamilifu.
Hata uliangalia magari ya mwanzo kabisa, ni tofauti kabisa na magari tuliyonayo sasa.
Kila kitu huwa kinaanza kikiwa na makosa na mapungufu mengi, kisha kuendelea kuboreshwa na kuwa imara zaidi.
Hata biashara, wengi leo wapo kwenye biashara ambazo ni tofauti kabisa na kipindi wanaanza.
Walipoanza walikuwa na mipango fulani, ila walipoingia sokoni wakagundua mipango yao haikuwa sahihi hivyo wakaiboresha.
Hilo pia lipo kwenye sanaa za kila aina, kuanzia uandishi, uchoraji n.k. Hakuna anayeanza akiwa na ukamilifu. Kila mswada wa kwanza huwa na mapungufu mengi, yanafanyiwa kazi na kuwa bora zaidi.
Sasa kwa nini wewe unajichelewesha kufanya unachotaka kwa kusubiri mpaka kila kitu kikamilike?
Unapaswa kuanza, kufanya ambacho kina mapungufu, kisha kuyaboresha.
Unaweza kuboresha makosa yoyote yake baada ya kuwa umefanya.
Lakini huwezi kuboresha kitu ambacho hakijafanyika.
Hatua ya kuchukua;
Ni vitu gani umekuwa unapanga kufanya ila umekuwa unaahirisha kwa sababu unaona bado hujawa na ukamilifu?
Amua sasa kufanya bila ukamilifu kisha kuendelea kuboresha.
Fanya chochote kile, kisha kiboreshe mpaka kiwe vile unavyotaka.
Usisubiri ukamilifu, bali anzia pale ulipo.
Ukamilifu siyo tukio, bali ni mchakato.
Tafakari;
Kusubiri ukamilifu ni njia nyingine ya kutoroka na kuahirisha kufanya kile unachojua unapaswa kufanya.
Ni wakati sasa wa kujiambia wazi kwamba hupaswi kuendelea kutoroka. Anzia popote pale, kisha endelea kuboresha.
Kocha.