2681; Usumbufu.

Kuna hiki kitu kimoja ambacho ndiyo unachotaka sana kukifikia kwenye maisha yako.
Ndani ya KISIMA kwa kila mmoja wetu kitu hicho ni uhuru wa kifedha, kwa ngazi ya ubilionea.

Katika safari ya kukiendea kitu hiki, kuna vingine vizuri vitakavyojitokeza na kuweza kukushawishi kwamba unapaswa kuvijali pia.

Lakini lazima uwe na umakini mkubwa sana, kwani chochote kinachokutoa kwenye lengo lako kuu ni usumbufu, hata kama kwa nje kitaonekana ni kizuri na muhimu kiasi gani.

Kuna njia kuu za kukufikisha kwenye kile unachokitaka sana ambazo kwa lengo letu ni biashara na uwekezaji.

Zitakuja njia nyingine zinazoonekana nzuri na rahisi zaidi, huku zikilipa kwa haraka.
Lakini mwisho wa siku zinaishia kuwa usumbufu, kwa sababu haziwi sahihi kwetu.

Kwenye maisha, lazima ukubali kwamba kuna kupata na kukosa. Ukipata kimoja umekosa kingine.
Hivyo inapokuja kwenye ndoto yako kuu, kuwa tayari kupoteza vingine vyote ili tu uweze kufikia ndoto hiyo.

Chochote ambacho hakiendani na ndoto yako kuu na njia ulizochagua kuifikia ni usumbufu kwako.

Na kwenye hii safari ya mafanikio, hakuna kitu chenye gharama kubwa kama usumbufu.
Hiyo ni kwa sababu usumbufu huwa hauji moja kwa moja kama usumbufu.
Bali unakuja kama fursa nzuri, inayoshawishi kweli kweli na kukufanya uone usipochukua hatua unapitwa.

Ni pale unapotoa umakini wako kwenye ndoto yako kuu na kuupeleka kwenye vitu vingine ndiyo unakuja kushtuka kwamba haikuwa sahihi.
Kwani fursa uliyoshawishika nayo inakuja kuwa siyo fursa na huku ukiwa umeacha ndoto yako kuu.

Tuchague kukomaa kwenye ndoto kubwa tuliyonayo na njia tulizochagua kuifikia. Kwa fursa nzuri zinazokuja kwetu, tujikumbushe ni usumbufu uliojificha kama fursa.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku iandike ndoto yako kuu na njia kuu za kuifikia ndoto hiyo.
Kisha jikumbushe hayo tu ndiyo muhimu, mengine yote ni usumbufu kwako.
Hata uone ni mazuri kiasi gani, ni hila za dunia kukuondoa kwenye kile kilicho bora zaidi.

Tafakari;
Dunia inaendeshwa na msukumo wa hofu ya kupitwa (FOMO – Fear Of Missing Out). Na ndiyo maana watu hujikuta wakihangaika na kila usumbufu, kwa sababu wanaona wasipofanya hivyo watapitwa.
Wewe unapaswa kuendeshwa na msukumo wa raha ya kupitwa (JOMO – Joy Of Missing Out), ukishachagua ndoto yako, pambana na hiyo na furahia pale mengine yanapokupita, maana hayo ni usumbufu kwako.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining