#SheriaYaLeo (186/366); Jali kuhusu watu ili kuwajua kiundani.
Hatari kubwa inayokukabili ni kudhani kwamba unawajua watu kiundani na unaweza kuwahukumu kwa haraka.
Hilo siyo sahihi, kila mtu unayekutana naye ana mambo mengi ambayo bado huyajui.
Kama wanavyosema, moyo wa mtu ni kichaka, una mengi ambayo huwezi kuyaona haraka.
Hivyo mtazamo unaopaswa kuwa nao kwa wengine ni kwamba kuna mengi bado hujayajua kuhusu wao.
Kubali kwamba una udhaifu katika kuwahukumu watu kwa kuangalia kwa nje tu kitu kinachokuwa siyo sahihi.
Kwa kujua na kukubali hili kunakupa fursa ya kuepuka udhaifu wako wa kuhukumu haraka na kuwajua watu kwa undani.
Na njia nzuri ya kuwajua watu kwa undani ni kupitia maongezi ya kila siku.
Pale unapoongea na mtu, weka umakini wako wote katika kumsikiliza.
Usiwe muongeaji sana, bali kuwa msikilizaji mzuri.
Watu huwa wanapenda sana kujieleza, wanapokutana na mtu anayewasikiliza kweli.
Kwa kuwasikiliza watu kwa umakini na wao kujimwaga mambo yote kwako, unapata fursa ya kuwaelewa vizuri na kwa undani.
Hivyo pale unapopata nafasi ya kuongea, unaongea yale anayotaka kusikia, kitu kinachokupa ushawishi mkubwa kwake.
Kadiri unavyowaelewa watu ndivyo unavyoweza kuwashawishi kwa urahisi zaidi.
Na njia rahisi ya kuwaelewa watu ni kuwa msikilizaji mzuri na makini.
Watu husema yote pale wanaposikilizwa kwa umakini.
Hivyo tumia sana njia hiyo kuwajua watu kiundani.
Sheria ya leo; Achana na mazoea yako ya kuhukumu watu haraka. Fungua fikra zako ili kuweza kuwaona watu kwa namna ya tofauti. Usidhani kwamba mnafanana au mna msimamo wa aina moja. Sikiliza kwa makini na hapo utapata fursa ya kuwaelewa vizuri.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji