2682; Hapana ni moja, ndiyo ni nyingi.
Unaposema hapana kwenye jambo moja, unakuwa umekataa jambo hilo moja.
Lakini pia hapana hiyo moja inazuia mengine mengi ya mbeleni.
Unaposema ndiyo kwenye jambo moja, unakuwa umesema ndiyo kwenye mambo mengine mengi ambayo hata huyaoni.
Kwa kusema ndiyo moja, watu wanachukulia umesema ndiyo kwenye mengi au utakuwa tayari kusema ndiyo kwenye mengine.
Hivyo utashangaa unaposema ndiyo kwenye kitu kimoja kidogo, kinakuja kingine kikubwa na kuendelea kuja hivyo kadiri unavyoendelea kusema ndiyo.
Huu ni mtego ambao wengi hunaswa, wanashawishiwa kusema ndiyo kwenye kitu kidogo, halafu matakwa yanaenda yakiongezeka.
Wanapokuja kushtuka wanajikuta wamekubali kitu ambacho awali wangekikataa.
Kama huna uhakika na kitu, ni bora kusema hapana. Hapana hiyo itakukosesha kitu kimoja, lakini itakuacha ukiwa na nafasi ya kufanya yaliyo sahihi.
Kukimbilia kusema ndiyo ili usipitwe na fursa, unaishia kujikosesha fursa nyingine nzuri zaidi za baadaye kwa sababu mahitaji ya kusema ndiyo zaidi huongezeka.
Kadhalika kama hujioni ukikifanya kitu kwa muda mrefu usikikubali kwa muda mfupi.
Maana hakuna kinachodumu kama mambo uliyotegemea ni ya muda mfupi tu.
Hatua ya kuchukua;
Usiwe mtu wa kukimbilia kusema ndiyo, jiridhishe kweli kabla hujaitoa ndiyo.
Na pale unapogundua ulisema ndiyo kimakosa au bila ya kuwa na uelewa, kuwa tayari kubadilika.
Usikubali kunasa kwenye kile kisichokuwa sahihi kwa sababu tu unaonyesha msimamo kwenye ndiyo yako ya awali.
Na pale unapokuwa unalazimishwa sana kutoa jibu la ndiyo au hapana kwa haraka, ni bora utumie hapana. Hata kama ni kukosa, utakosa kimoja huku ukiendelea kusa na fursa nyingi.
Tafakari;
Maneno mafupi, NDIYO na HAPANA yana nguvu kubwa ya kukujenga au kukubomoa. Ni maneno unayopaswa kuyatafakari kwa kina kabla hujayasema ili usinase kwenye mtego utakaokuwa kikwazo kwako.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining