2703; Onyesha kazi yako.

Kuota ni rahisi na bure, kila mtu anaweza kuwa na ndoto, ziwe ni ndogo au kubwa.

Kupanga ni rahisi na bure, kila mtu anaweza kuweka mipango mbalimbali, iwe ni midogo au mikubwa.

Ni kuchukua hatua ndipo palipo pagumu kweli kweli na penye gharama kubwa.

Na tena siyo tu kuchukua hatua mara moja, maana hilo wengi hufanya, bali kuchukua hatua kwa msimamo, kwa muda mrefu bila kuacha, haijalishi ni matokeo ya aina gani unapata.

Hilo linahitaji mtu ujitoe kweli kweli, linahitaji mtu uwe na nia hasa na usiwe mtu unayekata tamaa haraka.

Lakini ndiyo linalohitajika ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako na kufanikiwa.

Waambie watu wakupe ndoto zao na watakupa kwa haraka.
Waambie watu wakueleze mipango yao na utapewa vizuri tu.
Ila waambie watu wakuonyeshe kazi zao, wakuonyeshe hatua ambazo wanapiga na hapo utapewa sababu za kutosha.

Sababu hazijawahi kumpa mtu kile anachotaka, zaidi tu ya kumdanganya ili aridhike.
Sababu ni sumu inayowapumbaza wengi na kuwazuia wasipambane kupata wanachotaka.

Kama unayataka mafanikio, weka sababu pembeni na onyesha kazi yako.
Kipaumbele chako cha kwanza kinapaswa kuwa ni kuchukua hatua kwenye ndoto na mipango uliyonayo.

Usiwe tu mtu wa kuota na kupanga.
Bali kuwa mtu wa kuziishi ndoto zako na kutekeleza mipango yako.
Usijali sana unapata nini, bali jali sana unafanya nini.
Kaa kwenye mchakato sahihi na mengine yote yatakaa sawa.

Hatua ya kuchukua;
Mara zote weka uzito kwenye kuchukua hatua, kufanya kazi na kukaa kwenye mchakato.
Epuka sana kutumia sababu au visingizio.
Kuwa mtu wa kufanya.
Unaweza kuonyesha kazi au unaweza kutoa sababu.
Wewe onyesha kazi.

Tafakari;
Sababu ni rahisi kutoa, lakini ni ngumu kuonyesha.
Kazi ni ngumu kufanya, lakini ni rahisi kuonyesha.
Chagua ugumu na urahisi wenye manufaa kwako.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining