2704; Huhitaji kuomba ruhusa.
Sehemu kubwa ya malezi ambayo tumepitia ni kikwazo kikubwa sana kwenye safari yetu ya mafanikio.
Tumejengewa sana nidhamu ya woga kiasi cha kukosa uthubutu wa kufanya yale ambayo tunapaswa kufanya ili tufanikiwe.
Na eneo kubwa na lenye madhara makubwa ni kwenye kuomba ruhusa.
Tangu tukiwa watoto, tumefundishwa kuomba ruhusa kabla ya kufanya jambo lolote.
Ilianzia nyumbani mpaka shuleni.
Hata kitendo cha kutaka kwenda kujisaidia, ilikuta auombe ruhusa.
Japo ilikuwa kwa nia njema, maana kila mtu hawezi kujiamulia tu nini afanye kama anavyojisikia, bado hali hiyo imeleta madhara makubwa kwetu mpaka kwenye hali ya utu uzima.
Wengi sana wanajua nini wanataka na hatua gani wanapaswa kuchukua ili kupata hicho wanachotaka.
Lakini kwa kuwa hakuna wengine wanaofanya hivyo, wanakosa uthubutu wa kukifanya, maana wanaona wamekosa ruhusa.
Kadhalika watu wengi wamejikuta wakiendelea kufanya mambo ambayo hayana tija kabisa kwao. Ila hawathubutu kuyaacha kwa sababu ndivyo kila mtu anavyofanya, wanajiona hawana ruhusa ya kuyaacha.
Ni wakati sasa wa kuvunja ukomo huo uliojengewa tangu ukiwa mtoto.
Tambua sasa kwamba huhitaji kumwomba mtu yeyote ruhusa katika kuyaishi maisha yako.
Fanya chochote unachotaka kufanya au acha kufanya kile usichotaka kufanya bila ya kusubiri ruhusa ya yeyote.
Kama tu huvunji sheria za nchi na za asili, wewe fanya.
Huhitaji ruhusa ya yeyote yule ndiyo uwe na furaha.
Hicho ni kitu ambacho tayari una ruhusa ya kuwa nacho kwa namna unavyotaka wewe mwenyewe.
Huhitaji ruhusa ndiyo uweze kujijengea utajiri mkubwa.
Hayo ni maamuzi yako mwenyewe.
Chochote unachotaka kufanya ili uwe na aina ya maisha unayoyataka, tambua ni kitu kilicho ndani ya uwezo wako na ambacho huhitaji kusubiri ruhusa ya yeyote ndiyo ukifanye.
Mpuuze yeyote anayekuhadaa kwamba unahitaji ruhusa au anayekushangaa umethubutuje.
Ni maisha yako na maamuzi yako, usisubiri ruhusa ya yeyote.
Lakini lazima pia ukubali,
Kwamba unapoacha kuomba ruhusa,
Lazima uwe tayari kuyakubali matokeo,
Yawe ni mazuri au mabaya.
Siyo unakataa kuomba ruhusa,
Halafu unaanza kulaumu wengine kwa matokeo unayopata.
Hayo ni juu yako.
Hatua ya kuchukua;
Chochote unachotaka lakini bado hujakiendea, haijalishi ni sababu gani unajipa, unachosubiri ni ruhusa.
Kwa bahati mbaya sana, hayupo wa kukupa ruhusa.
Hivyo jipe ruhusa leo na uanze kufanya.
Usiendelee kupoteza tena muda kusubiri.
Tafakari;
Mamlaka yanakuja na wajibu.
Unaposhika mamlaka ya maisha yako maana yake pia umechagua kuwajibika na maisha hayo.
Usiwe tu mtu wa kuangalia unachotaka, angalia pia kukikosa na kuwajibika kwa hilo.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining