Rafiki yangu mpendwa,

Leo ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwangu.

Tarehe 28/05/1988 ndiyo siku ambayo nilizaliwa, hivyo leo tarehe 28/05/2022 nimetimiza miaka 34 ya kuwa hai hapa duniani.

Kwa miaka hiyo michache, nimejifunza mengi sana na pia nimekazana kuwa na mchango kwa wengine kadiri ya uwezo wangu.

Leo hii, katika kumbukizi ya kuzaliwa kwangu nimeona nikushirikishe mambo 3.4 ambayo ninayaamini sana kwenye safari hii ya mafanikio.

Hayo ni mambo ambayo ninayaamini bila ya shaka yoyote na yamekuwa na mchango mkubwa kwa pale nilipofika sasa.
Na ndiyo nitakayoendelea kuyasimamia katika kuziendea ndoto zangu kubwa mbili nilizonazo.

Kabla sijaingia kwenye hayo ninayoamini, nikukumbushe ndoto zangu kubwa mbili ninazozipigania na hatua ninazoendelea nazo.

Nilishaweka wazi na nimekuwa narudia kwamba nina ndoto kubwa mbili kwenye maisha yangu.
Ndoto ya kwanza ni kuwa bilionea (kwa kipimo cha dola) mpaka kufikia mwaka 2030.
Na ndoto ya pili ni kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040.

Maendeleo ya ndoto hizo kubwa mbili ni kwa sasa nipo kwenye mchaka mchaka wa kufikia ubilionea na hilo litasababisha unikose sana.
Ndoto ya uraisi nitaanza kuifanyia kazi baada ya kukamilika kwa ndoto ya ubilionea.

Kwa sasa akili, nguvu, hisia na umakini wangu wote upo kwenye kupambana kufikia ubilionea.
Na ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba nitafikia ndoto hizo mbili, maana nitazipambania bila kukata tamaa.
Ni labda nitazifikia au nitakufa nikiwa nazipambania, hakuna mnadala wa hilo.

Baada ya kukukumbusha ndoto hizo mbili na maendeleo yake, sasa twende kwenye mambo 3.4 ambayo ninayaamini sana kwenye hii safari ya mafanikio.

1. KAZI.

Jambo la kwanza ninaloliamini sana kwenye hii safari ya mafanikio ni kazi.
Ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba rafiki wa kweli na ambaye hawezi kukusaliti kwa namna yoyote ile ni kazi.

Ipende kazi na kuwa tayari kuweka kazi na itakupa chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Sisemi haya kwa kubahatisha, bali kwa sababu ni utayari wangu wa kuweka kazi kwa juhudi kubwa ndiyo umenifikisha hapa nilipo.

Nikupe mfano mdogo ambao ushahidi wake upo wazi.
Tangu tarehe 01/01/2015 niliamua kwamba nitakuwa naandika kila siku bila ya kuacha.
Mpaka kufika leo ni siku 2705 za kuandika kila siku bila kuacha.
Na kielelezo kipo kwenye makala za kurasa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, zipo kwa mlolongo wa namba.

Sijaweza kufanya hilo kwa sababu kila siku nilikuwa najisikia kuandika. Kuna siku ambazo sikuwa najisikia kabisa kuandika.
Lakini kwa kuwa naamini sana kwenye kazi, sikuwa na namna bali kuandika.

Hiyo ni sehemu ndogo sana ya kazi ninayoweka kila siku, lakini inakufanya uelewe kile ninachosema ni nini.

Ninachotaka kwako rafiki yangu ni ujenge imani kubwa kwenye kazi.
Ipende sana kazi.
Weka juhudi kubwa kwenye kazi.
Na kazi haitakutupa,
Kazi itakulipa.

Waruhusu watu wakuzidi akili, elimu, fedha, koneksheni na hata vipaji.
Lakini kamwe kamwe usimruhusu mtu yeyote akuzidi kwenye kazi.

Kwa chochote unachofanya, hakikisha unajijengea sifa (kwa vitendo na siyo maneno) kama mtu unayeweka juhudi kubwa kwenye kazi kuliko watu wengine wote.
Fanya hivyo na utashangaa jinsi fursa nzuri zitakavyokuja kwako.

Tahadhari;
Nilichokuambia hapa kuhusu kazi kinaenda kinyume kabisa na jinsi jamii inavyokuambia kuhusu kazi.
Jamii inakuhadaa usifanye kazi sana.
Inakuambia kuna njia za mkato.
Inakuambia usifanye kazi kwa nguvu na juhudi, bali kwa akili tu.
Huo wote ni ulaghai na kama utausikiliza rafiki yangu, maisha yako yataendelea kuwa magumu na hautafanikiwa.

2. MAARIFA.

Maarifa ni jambo jingine muhimu sana ninaloliamini kwenye hii safari ya mafanikio.
Ni maarifa ndiyo yaliweza kubadili kabisa mtazamo wangu kuhusu maisha na mafanikio tangu mwaka 2012.
Na tangu kipindi hicho nimesoma na kusikiliza vitabu zaidi ya elfu moja.
Ndiyo, vitabu zaidi ya elfu moja.

Kila mtazamo nilionao leo, kila ninachojua leo, havitokani na akili zangu, bali vinatokana na maarifa mengi ambayo nimekuwa nayakusanya kila siku.

Usomaji wa vitabu ni kipaumbele cha kwanza kwangu.
Baada ya kugundua akili ni kama tumbo, nilidhamiria kutokuulisha mwili kama sijailisha akili.
Hivyo kabla sijala chakula, lazima kwanza nisome kitabu.

Na hili pia lina ushahidi wa wazi, wa vitabu vingi nilivyosoma na kuchambua vinavyopatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA (www.t.me/somavitabutanzania)

Ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba hakuna tatizo unalopitia sasa kwenye maisha yako ambalo halina suluhisho lililoandikwa kwenye vitabu.
Unachohitaji ni kusoma vitabu sahihi ili kutoka pale ulipokwama sasa.

Wito wangu kwako wewe rafiki yangu ni uamini kwenye maarifa na kama ambavyo unalilisha tumbo lako kila siku, basi pia lisha akili yako chakula chake ambacho ni maarifa.

Na maarifa ninayoeleza hapa ni yale unayopata kupitia kusoma au kusikiliza vitabu.
Makala hazihesabiki, japo zinaweza kuwa na mafunzo mazuri.
Vitu unavyojifunza kwenye mitandao ya kijamii pia havihesabiki.
Fanya vyote kwa kadiri unavyoweza, lakini cha msingi kabisa ni VITABU.
Soma vitabu, sikiliza vitabu.

Kingine muhimu sana kwenye usomaji ni kuchukua hatua.
Haitoshi tu kusoma, unapaswa pia kufanyia kazi yale uliyojifunza.
Tena kuyafanyia kazi yakiwa bado ni ya moto kabisa.
Hivyo unapojifunza kitu kipya kupitia usomaji wa vitabu, kiweke kwenye matendo mara moja.
Kwa njia hiyo kila mara utakuwa na mawazo mazuri na ya kibunifu yatakayokupa manufaa makubwa.

Tahafhari;
Jamii haitakuruhusu usome vitabu.
Itakuhadaa na vipindi vya tv,
Itakunasa kwenye mitandao ya kijamii,
Na itakufanya ubeze maarifa yaliyopo kwenye vitabu kwamba hayafanyi kazi.
Jamii itakuweka bize na mambo yasiyo na tija ili tu usisome vitabu.
Kwa sababu unakuwa rahisi kutawaliwa na kutumiwa kwa manufaa ya wengine kama husomi vitabu.
Ukiiendekeza jamii kwenye hili, utabaki kwenye maisha duni.

3. WATU.

Kwenye safari ya mafanikio, watu wana mchango mkubwa sana.
Lakini siyo watu wote ni sawa na sahihi kwako.

Watu ni jambo jingine ninaloliamini sana kwenye hii safari ya mafanikio.
Na siyo kila aina ya watu, siyo watu wote, bali watu sahihi kwako.

Tukianza na kanuni ya msingi kabisa; maisha yako ni wastani wa maisha ya watu watano unaotumia nao muda wako mwingi.

Hii ni sheria ambayo hakuna mwenye nguvu ya kuivunja.
Wachukue watu watano wa karibu kabisa kwako, wale ambao unatumia nao muda wako mwingi, kisha yaangalie maisha yao na yako.
Utagundua vitu vingi sana mnafanana.
Unadhani hilo limetokea kwa bahati?
Hapana, limetokea kwa makusudi kabisa.
Unakuwa kama wale unaowapa nafasi kwenye maisha yako.

Hivyo jambo muhimu sana la kuzingatia hapa ni kuchagua aina sahihi ya watu wa kuwa nao.
Watu ambao tayari wameshafika kule unakoenda au ndiyo wanaelekea huko.
Watu ambao wana ndoto kubwa na kila siku wanapambana kuzifikia.
Watu ambao siyo wa kukata tamaa.
Watu ambao wanapenda kuona wengine wanafanikiwa.

Zungukwa na watu wasio na sifa hizo na hakuna hatua utapiga.
Utaweka juhudi kubwa sana, lakini utaishia kubaki pale pale ambapo wenzako wapo.

Tunategemeana sana kwenye hii safari ya mafanikio.
Lakini siyo watu wote wanaotufaa.
Hivyo unapaswa kuchagua watu sahihi kwako na kuambatana nao.

Tahadhari;
Jamii imejaa watu wa kawaida ambao hawawezi kupata mafanikio makubwa.
Wengi wa wanaokuzunguka ni wa kawaida sana na hawatapata mafanikio makubwa.
Ni wakati sasa wa kuwabadili watu unaowapa muda wako.
Tafuta watu waliofanikiwa sana au ambao wanapambana kufanikiwa na hao ndiyo unapaswa kutumia nao muda wako mwingi.
Na kama huwezi kupata watu wa aina hiyo, basi tumia muda wako mwingi kwenye vitabu na kazi, ukijifunza ili kuwa bora na kuweka juhudi zaidi kwenye kazi.
Haitachukua muda utaanza kuwavuta watu sahihi kwako.
Utakapoanza kukaa mbali na watu wasio sahihi kwako, hawatakuacha salama.
Watakuambia umebadilika,
Watasema una dharau
Na mengine mengi.
Wapuuze kama unayataka mafanikio.

3.4. MUDA.

Watu wote duniani tuna muda sawa.
Hata mtu tajiri kuliko wote duniani, bado ana masaa 24 kwa siku kama ambavyo masikini wote wanayo.

Ni kwenye muda pekee ndipo penye demokrasia ya kweli duniani.
Ndiyo kitu pekee ambacho wote tumepewa kwa usawa.

Sasa kwa kuwa tumepewa kwa usawa, ila wapo ambao wanafanya makubwa sana kwenye muda huo huo, ina maana kuna vitu wanafanya kwa utofauti.

Na hapo ndipo muda unapokuwa muhimu sana.
Na ndiyo maana muda ni kitu kingine ninachokiamini mno.

Naamini ukitumia muda wako vizuri, utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Kwa yote ambayo nimeweza kufanya, ni kwa sababu nimekuwa nakazana kutumia muda wangu vizuri.

Na siri kuu ya kutumia muda vizuri ni kusema HAPANA kwenye mambo yote ambayo hayana mchango kwenye maisha yako na mafanikio unayotaka.

Kwa mfano, haya ni mambo ambayo nilishasema hapana kwenye maisha yangu na kutokuyafanya kumeokoa muda wangu mwingi.
1. Kufuatilia habari kwa tv, redio, magazeti na vyombo vingine vya habari.
2. Matumizi ya mitandao ya kijamii, sipo kwenye mtandao wowote wa kijamii.
3. Ushabiki wa mchezo wa aina yoyote ile, sifuatilii michezo yoyote.
4. Ulevi na starehe mbalimbali, situmii kilevi chochote.
5. Vikao na shughuli nyingi za kijamii, sihudhurii mambo ambayo siyo muhimu kabisa.

Kwa kusema hapana kwenye hayo, nabaki na muda mwingi ambao naweza kuutumia kwenye mambo yenye tija zaidi.

Rai yangu kwako rafiki yangu ni hii, linda sana muda wako. Tumia neno HAPANA kwa yote yasiyokuwa na mchango kwenye mafanikio unayoyataka.

Tahadhari;
Jamii ina mbinu nyingi sana za kunasa muda wako.
Inakulazimisha ufanye yale ambayo kila mtu anafanya ndiyo uonekane wa kawaida.
Chagua kama unataka kuwa wa kawaida na usifanikiwe.
Au kuwa wa ajabu na ufanikiwe.
Huwezi kufanikiwa bila kuonekana wa ajabu kwenye jamii.
Kwamba hufuatilii habari, haupo kwenye mitandao na hushabikii chochote!
Wengi watakuona una tatizo, ila wao ndiyo wenye tatizo kubwa zaidi.

Rafiki yangu, kutoka ndani ya moyo wangu kabisa hayo ni mambo ninayoyaamini bila ya shaka yoyote ile.
Ninakusihi ujenge imani kubwa kwenye mambo hayo na kuyasimamia kila siku bila ya kutetereka.
Na kwa hakika utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Karibu tuendelee kuwa pamoja kwenye hii safari. Njia za kuendelea kushirikiana ni kama ifuatavyo;
1. Makala za bure kabisa ambazo ni nzuri na zenye manufaa zinaendelea kupatikana kwenye AMKA MTANZANIA; www.amkamtanzania.com
2. Vitabu vizuri vya mafanikio vinapatikana kwenye SOMA VITABU TANZANIA; www.somavitabu.co.tz
3. Chambuzi za vitabu vizuri zinapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA; www.t.me/somavitabutanzania
4. Huduma za ukocha zinapatikana kwa uchache sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA; www.kisimachamaarifa.co.tz

Karibu rafiki yangu tuambatane pamoja kwenye safari hii ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.