2706; Kupanga na kufanya.
Kwa ujumla, mchakato mzima wa mafanikio unategemea sana kwenye kupanga na kufanya.
Ni kitu rahisi lakini chenye nguvu kubwa sana ya kuamua mtu afanikiwe au ashindwe.
Watu wengi huwa wanapanga lakini hawafanyi.
Kupanga ni rahisi, kufanya siyo.
Hivyo watu wana mipango mingi, lakini hawaitekelezi.
Watu wengine wanafanya bila kupanga.
Hawa mara nyingi huendeshwa na hisia.
Chochote kinachoteka hisia zao ndiyo wanakifanya kwa wakati huo.
Hawa pia huwa hawafanikiwi kwa sababu hawafanyi chochote kwa muda wa kutosha kuona matokeo.
Hisia huwa zinadumu kwa muda mfupi, hivyo muda huo mfupi unapopita na hisia kuisha, wanaacha kufanya.
Ni wachache sana ambao wanapanga na kufanya kama walivyopanga ndiyo wanaofanikiwa kupata mafanikio makubwa.
Hawa wanatenga muda wa kutosha wa kupanga kwa kina, wakiwa wanajua nini hasa wanachotaka na wanakipataje.
Kisha wanatekeleza mipango yao kama walivyoiweka bila ya kuruhusu kitu chochote kile kiwakwamishe.
Inyeshe mvua au liwake jua, wao watatekeleza kama walivyopanga.
Hawaruhusu sababu yoyote ile kuwa kikwazo kwao.
Wakati wengine wakiona hawataki kujitesa, wanaofanikiwa wanajua wasipojitesa kwa kufanya waliyopanga, dunia itawatesa kwa kuwa na maisha duni.
Hatua ya kuchukua;
Weka mipango ya kufanyia kazi ili kupata kile unachotaka na kisha fanyia kazi mipango hiyo.
Utakutana na mengi yatakayokukwamisha na kukuhadaa uachane na mipango yako, lakini usikubali.
Wewe endelea kufanya kama ulivyopanga.
Tafakari;
Kupanga lakini usifanye ni uvivu, haijalishi unatumia sababu gani kushindwa kufanya, uvivu ndiyo kitu kikubwa kwako.
Kufanya bila ya kupanga ni mhemko, haijalishi umeanza kwa mbwembwe kiasi gani, hutafika mbali.
Ni kupanga na kufanya kama ulivyopanga ndiyo nidhamu sahihi itakayokuwezesha kupata kile unachotaka.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining