2748; Yasiyo na thamani.

Mwandishi mmoja amewahi kuandika; muda ndiyo demokrasia ya kweli.
Ni muda pekee ndiyo wenye usawa kwa watu wote.

Kila mtu anayapata msaa 24 pekee kwenye siku yake.
Hakuna mwenye uwezo wa kuongeza hata dakika moja ya ziada kwenye muda wake.

Katika muda huo huo wenye uhaba, kuna watu wanafanikisha kufanya makubwa.
Na kuna wengine wengi ambao wanalalamika kwa kukosa muda.

Kama huwezi kutumia muda wako vizuri, hakuna namna itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Hatua ya kwanza ya kutumia muda vizuri ni kusema HAPANA kwenye mambo mengi.

Na utaweza kusema HAPANA kama tayari unajua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako.

Kwa kujua unachotaka, unakuwa umejua nini cha kufanya ili kupata unachotaka.
Chochote ambacho hakina mchango kwenye kufika kule unakotaka kufika hakina thamani yoyote.

Unapaswa kuachana na mambo yote yasiyo na thamani ili utumie vizuri muda wako kwenye mambo yenye tija na thamani kubwa.

Hatua ya kuchukua leo;
Kagua matumizi yako ya muda unayofanya sasa.
Orodhesha yote unayofanya kisha angalia ni yapi yanakusogeza karibu na malengo yako.
Hayo ndiyo unapaswa kuyazingatia na kuyapa kipaumbele zaidi.

Tafakari;
Muda ni rasilimali yenye uhaba na thamani kubwa.
Muda ndiyo kitu kilichojenga maisha yetu.
Upo hapo ulipo sasa kutokana na matumizi yako ya muda huko nyuma.
Na kesho yako inatengenezwa na matumizi yako ya muda leo.
Kuwa makini na muda, una nguvu kubwa kwenye maisha yako.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed