2768; Kujitetea kusiko na maana.

Kama kuna mtu ambaye anapata matokeo ya tofauti na yale unayopata wewe, ni kwa hakika anafanya vitu vya tofauti na unavyofanya wengi.

Na kama ni matokeo mazuri ambayo hata wewe ungependa kuyapata, kujifunza kwa mtu huyo kuna nguvu kuliko tu kumbeza au kujipa sababu kwa nini yeye ameweza na wewe umeshindwa.

Wengi wanapoona wenzao wanafanya vizuri kuliko wao, badala ya kujifunza kwa watu hao, wanaanza kujitetea.

Wanajiambia wengine wameweza kwa sababu fulani ambazo zinawaweka kwenye manufaa zaidi huku wao wakishindwa kutokana na sababu fulani zinazowaweka kwenye hasara au ugumu.

Mfano, mwenzako ambaye mmeanza naye kazi au biashara pamoja, anapofanikiwa kuliko wewe, unaishia kujiambia ni kwa sababu alipata manufaa fulani ambayo wewe hukupata.
Landa alipata ‘koneksheni’ fulani, au unajiambia hana majukumu makubwa kama wewe n.k.

Kote huko ni kujidanganya tu kusiko na maana. Kwa sababu kwa nje unaweza kuona kama mtu ana manufaa fulani anayapata kuliko wewe.
Lakini ungepewa nafasi ya kuingia ndani yao, ungegundua magumu na makubwa wanayopitia kuliko hata ya kwako.

Ninachotaka kukuambia wewe rafiki yangu ni kama kuna hatua ambazo wengine wamefikia ila wewe bado, chochote unachojitetea nacho hakina maana.

Kitakachokusaidia ni kujifunza kutoka kwa watu hao ili uweze kupata matokeo bora kama wao.
Huwezi wala hupaswi kuiga kila ambacho wengine wanafanya, kwa sababu kufanya hivyo hakutakupa matokeo kama yao.

Badala yake unapaswa kujifunza kutoka kwa wengine, kuona matokeo gani yanawezekana na namna gani unapaswa kufanya ili kupata matokeo bora kabisa.

Hatua ya kuchukua;
Kokote unakotaka kufika na maisha yako, angalia wale wote ambao tayari wameshafika, kisha jifunze kutoka kwao.
Weka pembeni utetezi wowote unaojipa kwa nini wao wameweza na wewe hutaweza.
Jua kama wao wameweza, hata wewe utaweza pia. Ni kujifunza na kuchukua hatua sahihi ndicho unachokihitaji.

Tafakari;
Benjamin Franklin amewahi kusema; Baadhi ya watu wanapaswa kufanikiwa ili kuwaaminisha wengine kwamba mafanikio yanawezekana.
Jifunze kwa waliofanikiwa zaidi yako na wewe kuwa sehemu ya wengine kujifunza ili nao wapige hatua zaidi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed