#SheriaYaLeo (297/366); Nafsi iliyopotea.
Kila mtu huwa ana nafsi yake ambayo ameipoteza.
Hilo linatokana na mtu kuchagua kuwa kama vile ambavyo watu wanataka awe na siyo kama anavyosukumwa kuwa kutoka ndani yake.
Wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kuondokana na hali ya mgando unayokuwa nayo, vile unavyojiweka ili kuwaridhisha wengine.
Unapaswa kuwa tayari kubadilika na kurejea kwenye nafsi yako uliyoipoteza.
Ni kwenye nafsi hiyo ndipo penye nguvu kubwa kwako.
Kwa kurudi kwenye nafsi yako iliyopotea, watu watakushangaa na kushindwa kukuelewa. Watakuona kama umepotea.
Usijali kuhusu hilo, huhitaji kueleweka na kila mtu.
Ili ufanikiwe, unachohitaji ni kuwa wewe.
Kadiru watu wanavyoshindwa kukuelewa ndivyo unavyokuwa na nguvu juu yao.
Maana hawawezi kukuzoea katika hali hiyo.
Hivyo anza kwa kufanya tofauti na ulivyozoeleka.
Kama ulikuwa mtu wa kujilinda anza kushambulia.
Kama ulikuwa mpole kuwa mkali.
Chochote ambacho umekuwa unakandamiza ndani yako ili tu kuwaridhisha wengine, ni wakati wa kukiachilia.
Kwani hicho ndiyo chenye nguvu kubwa ya kukuwezesha kufanikiwa.
Chochote unachoficha au kukandamiza ndiyo kinazuia usitoe nguvu zako kubwa na za kipekee.
Ni wakati sasa wa kuachilia kila kilicho ndani yako ili uweze kujitofautisha na wengine na kufanya makubwa zaidi.
Sheria ya leo; Rejesha nafsi yako iliyopotea. Rudisha ule msukumo mkubwa wa ndani yako ambao umekuwa unaukandamiza. Huo ndiyo wenye nguvu kubwa ya mafanikio kwako.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji