Rafiki yangu mpendwa,
Leo ni siku ya Sensa ya watu na makazi nchini Tanzania.

Asubuhi hii wakati naelekea kwenye shughuli zangu, nimekutana na makarani wengi wa Sensa wakiwa wanaingia kwenye mitaa kwa ajili ya kuanza kazi yao.

Hilo limenikumbusha miaka 10 iliyopita, mwaka 2012 ambayo Sensa ya mwisho ilifanyika.

Nilikuwa mmoja wa makarani wa Sensa na naikumbuka siku yenyewe jinsi ambavyo niliwahi kwenye eneo langu na kuanza kutekeleza wajibu huo.

Kuwaona makarani hawa leo imenipa picha ya nilipokuwa miaka 10 iliyopita.

Imenifanya niangalie haraka tofauti ya miaka 10 iliyopita na sasa, je nimepiga hatua kiasi gani?

Kwa haraka sana nimeona kuna mengi nimeweza kupiga hatua ukilinganisha leo na miaka 10 iliyopita.

Miaka 10 iliyopita sikuwa nimeandika kitabu hata kimoja, ila mpaka sasa nimeandika vitabu zaidi ya 20.

Miaka 10 iliyopita sikuwa na hadhira ya watu wanaofuatilia kazi zangu, ila mpaka sasa nina hadhira ya watu zaidi ya elfu 10 ambao wanafuatilia kazi zangu moja kwa moja.

Miaka 10 iliyopita sikuwa nimeuza kitabu kwa mtu hata mmoja, ila mpaka sasa nimeuza vitabu kwa watu zaidi ya elfu 5.

Miaka 10 iliyopita sikuwa nimetoa huduma ya ukocha kwa mtu hata mmoja, ila mpaka sasa nimetoa huduma ya ukocha kwa watu zaidi ya elfu 1.

Miaka 10 iliyopita nilikuwa nimesoma vitabu vitatu tu vya maendeleo binafsi, ila mpaka sasa nimesoma vitabu zaidi ya elfu 1 vya maendeleo binafsi.

Rafiki, sikuambii haya kujitamba au kukuonyesha mimi ni bora kuliko wewe.
Bali nakushirikisha hapa safari yangu kwa miaka 10.

Ambapo yote hayo nimeweza kuyafikia kwa kitu kimoja tu; KAZI.

Hakuna ambapo nimewahi kupewa upendeleo ndiyo nikakamilisha hayo.

Hakuna ambapo niliwahi kupewa mtaji au aina nyingine ya msaada wa moja kwa moja kukamilisha hayo.

Yote ni matokeo ya kuweka KAZI kwa juhudi kubwa bila kuacha.

Kitu ambacho nimekuwa nakuambia mara kwa mara, nikikusihi sana ujinengee utaratibu huu mzuri wa kupenda kazi.

Sasa naiangalia miaka mingine 10 iliyo mbele yangu, ambayo hii lengo lake ni moja tu, kufikia ubilionea.
Na hilo sina shaka nalo, kwa sababu nina uhakika na kitu kimoja ninachoweza kukitoa, ambacho ni kazi.

Na baada ya hii miaka 10 tuliyopo sasa kuisha, nitakwenda kwenye lengo jingine kubwa la pili nililonalo. Ambalo kama umekuwa mfuatiliaji mzuri wa kazi zangu unalijua.
Nalo pia sina wasiwasi nalo, maana najua kitu kimoja ninachoweza kukitoa kwa uhakika, ambacho ni KAZI.

Imetosha kwa leo kwa upande wangu rafiki.
Sasa ni wakati wa mimi kusikia kutoka kwako.
Unaionaje miaka 10 iliyopita kwa upande wako?
Unakumbuka nini kwenye siku ya sensa ya mwaka 2012?
Wakati huo wa sensa ya 2012 ulikuwa wapi na leo sensa ya 2022 uko wapi?
Unapanga kuwa wapi kwenye sensa ijayo ya mwaka 2032?
Karibu unishirikishe haya rafiki yangu, tujadiliane namna bora ya kwenda kuyafanyia kazi hayo.

Nasubiri kusikia kutoka kwako rafiki yangu.

Kocha.