2795; Usifanye kazi, bali cheza.
Elon Musk, mtu tajiri kuliko wote duniani kwenye zama hizi, anafanya kazi kwa juhudi kuliko watu wengine wote.
Pamoja na utajiri mkubwa alionao, ambao hata akiamua alale kila siku au hata kufanya kila aina ya starehe hawezi kuumaliza, bado kazi ni kipaumbele kikubwa kwake.
Bado anakuwa tayari kukesha kwenye viwanda vyake kuhakikisha uzalishaji ni wa viwango vya juu kama anavyotaka.
Bado anaendelea kuahidi makubwa na kujisukuma kuyatekeleza.
Hayo yote yanawezekana kwa Musk kwa sababu hachukulii anachofanya kama kazi. Bali anachukulia kama mchezo pendwa kwake.
Anaangalia kile anachochangia kwenye dunia na ndiyo kinamsukuma zaidi.
Unachukulia kitu ni kazi pale sababu pekee inayokusukuma kukifanya ni kupata pesa, tena ile ya kuendesha maisha.
Sisemi kuna ubaya wowote kufanya kitu ili upate pesa, ila kama ndiyo sababu pekee basi jua umeshapotea.
Umeshapotea kwa sababu ukiingia kwenye ushindani na ambaye hasukumwi na pesa, atakumaliza kabisa.
Ukipata pesa kidogo utakimbilia kufanya starehe, maana kile unachofanya siyo starehe kwako.
Wakati mshindani wako anachofanya ndiyo starehe yake.
Unadhani atakuacha salama?
Fanya unachopenda au penda unachofanya ni ushauri maarufu na wa muda mrefu, ambao watu wamekuwa hawaupi uzito unaostahili.
Naweza kukuhakikishia ya kwamba sababu ya kwanza ya watu kushindwa kufanikiwa au kupata anguko baada ya kufanikiwa kidogo ni kutokupenda kile wanachofanya.
Kama kuna kingine upo tayari kukifanya kuliko kile kikuu kinachokupa mafanikio, jua tayari umeshashindwa au hata ukifanikiwa ni kwa muda tu, angulo ni la uhakika.
Yaani kama kuna kitu kingine ungekuwa unapenda kufanya zaidi ya kile kikuu unachofanya kupata fedha na mafanikio, unakuwa umegawanyika.
Unakuwa hujazama kweli kwenye hicho kitu na hilo kitakuwa kikwazo kwako.
Mwanzoni unaweza kuona haina shida, kwa kuwa una shida, zinakusukuma ufanye zaidi.
Ni pale shida zako ndogo ndogo zinapoondoka ndipo sasa matatizo makubwa yanaibuka, matatizo ambayo yatakuondoa kabisa kwenye njia ya mafanikio uliyopo.
Rafiki, hakuna mbadala wa kupenda sana kile unachofanya kama unataka kikupe mafanikio makubwa.
Hicho ndiyo kinapaswa kuwa namba moja kwako.
Ambacho hakuna kingine kinakushawishi uachane na hicho ili kwenda kukifanya.
Kuna kauli ya Kiingereza inayosema; GO ALL IN. Yaani uingie mzima mzima, usijibakishe hata kidogo.
Hiyo ndiyo namna pekee ya kujihakikishia mafanikio makubwa kwenye maisha yako na ambayo yatadumu kweli.
Pale unapojiona kuna vitu vingine vinavyoweza kukutoa kwenye kile ulichochagua, jua wazi umejiweka eneo ambalo mafanikio yatakuwa magumu sana kwako.
Hatua ya kuchukua;
Jitathmini kwa wiki moja na mwezi mmoja uliopita, ni vitu gani vimefanikiwa kukutoa kwenye kile kikuu ulichochagua kufanya?
Ni vitu gani vimeweza kukushawishi uahirishe kufanya kile unachopaswa kufanya kila siku kwenye mchakato wako?
Kama kipo chochote ambacho kimewahi kukukwamisha, basi jua upo kwenye hatari ya kutoyafikia mafanikio makubwa.
Au hata ukiyafikia basi utakuja kukutana na anguko kubwa.
GO ALL IN ni msingi unaopaswa kujipima nao kila wakati.
Tafakari;
Kama starehe au changamoto yoyote ya kimaisha inaweza kukuondoa kwenye mchakato wa kile unachopaswa kufanya kila siku ili ufanikiwe, haupo kwenye kundi la wale watakaopata mafanikio makubwa na wakadumu nayo.
Unaweza kujifariji vile utakavyo, lakini ukweli utabaki kuwa hivyo.
Maana hata asili inakudhihirishia wazi. Hujawahi kuahirisha kupumua, mapigo ya moyo au kula kwa sababu ya kitu chochote kile. Kwa sababu hivyo ni vitu muhimu, unavipa kipaumbele kikubwa.
Kwa nini usiyape mafanikio yako kipaumbele cha aina hiyo?
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed