#SheriaYaLeo (299/366); Chunguza mizizi ya hisia zako.

Kila hisia unazokuwa nazo, huwa zinakuwa na mizizi yake ambayo huwa haionekani wazi.
Ni mpaka uchunguze kwa kina ndiyo utaweza kujua chanzo halisi cha hisia unazokuwa nazo.

Kwa mfano umepatwa na hasira, unapaswa kuacha hisia hizo zitulie, kisha kuchunguza nini kimezisababisha.
Kama zimesababishwa na kitu kidogo na kisichokuwa na uzito, maana yake kuna sababu nyingine zilizojificha nyuma ya hayo.

Mara nyingi inakuwa ni hisia za wivu na wasiwasi zimejificha ndani ya mtu na hataki kuzikubali au kuzikabili.
Unapaswa kuchimba ndani ili kujua chanzo halisi cha kila hisia unazokuwa nazo.
Unaweza kuwa na kitabu unachotumia kwenye zoezi hili, kila unapokuwa na hisia kali, unakaa chini na kuandika chanzo halisi cha hisia hizo.

Hatari kubwa kwenye zoezi hili ni ufahari wako, ambao utakufanya ushindwe kuwa mkweli kwako.
Kujidanganya kunaweza kukupa faraja ya muda, lakini itakuzuia kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Kujidanganya na kutokujua chanzo halisi cha hisia zako kutakufanya uwe mtu wa kujihami na kujitetea kwenye kila jambo.

Mara zote tafuta upande usiofungamana ili uweze kuona kila hisia na kila matendo unayokuwa nayo na chanzo chake.
Hilo litakuwezesha kuzijua kwa kina na kuzitawala hisia zako kwa namna ambayo hazikusumbui.
Utaweza kutatua kila tatizo na changamoto unazokuwa nazo kwa utulivu na kuweza kupiga hatua kubwa.

Sheria ya leo; Jijengee tabia ya kuchunguza kwa kina hisia zako. Hilo litakuwezesha kuondokana na mambo madogo madogo yasiyo na tija ila yanaibua hisia kali kwako na kuwa kikwazo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji