2797; Tabu iko pale pale.

Katika kutoa mafunzo kwenye timu ya wafanyakazi wa taasisi fulani, niliendesha zoezi la kila mmoja kutoa mawazo yake nini kifanyike ili kukuza mauzo mara mbili ndani ya mwaka mmoja.

Mawazo mengi mazuri yalitolewa, lakini moja ambalo lilijirudia rudia ni kupunguza bei ili wateja wengi zaidi waweze kumudu kununua.

Lilikuwa wazo zuri, kwa sababu huwa nasisitiza kila wazo ni zuri, lakini kwenye utekelezaji lazima kuchuja.

Na hapo niliwauliza kama kweli wanaamini bei ndiyo kikwazo kikuu.
Nikawauliza hao wateja ambao kwa sasa tayari wapo kwa bei hiyo hiyo wamepatikanaje?
Na wanashindwaje kutafuta wateja wa aina hiyo zaidi?

Kitu nilichowaeleza ni kwamba, ndiyo, bei inaweza kuwa kikwazo kwa baadhi ya wateja, lakini biashara haiwezi kuwa ya kila mteja. Kama tayari kuna wateja kwa bei hiyo hiyo iliyopo, basi upo uwezekano wa kupata wateja wengine wengi zaidi.

Na nikaendelea kuwasisitiza kwamba kufanya biashara ni tabu na hakuna namna unaweza kuiepuka.

Kwa mfano ukipunguza bei, utakuwa umeondoa tabu ya kutafuta wateja, maana kwa bei rahisi watakuja wengi. Lakini utakuwa umehamishia tabu kwenye kulipwa. Wateja wa bei rahisi watakusumbua sana kwenye kulipa kwa wakati au kuthamini unachouza.

Ukiwek bei ya juu, utapata tabu sana kuwafikia wateja na kuwashawishi, lakini ukishawapata, utafurahi kuwahudumia, maana wanalipa kwa wakati na wanathamini kile wanacholipia.

Nikawapa mfano wa mwisho, kuna biashara mbili, A na B zote zinauza huduma moja.
A inatoza mteja tsh elfu 10 kupata huduma na ina wateja 400.
B inatoza mteja tsh elfu 20 na ina wateja 200.
Biashara zote mbili zina mauzo ya tsh milioni 4, lakini unafikiri nani ana tabu zaidi?
Yenye wateja 200 au 400?

Naamini umepata picha hapo.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kuwa tabu iko pale pale, unachopaswa ni kuchagua tabu gani unataka. Ya mwanzoni au ya mbeleni.
Kwa biashara unayofanya, chagua tabu yako, ikubali, ipokee na pambana nayo.

Tafakari;
Kama kungekuwa na njia rahisi ya mafanikio isiyohusisha kazi, isingekuwa siri bali bayana kwa kila mtu.
Yeyote anayekuambia kuna iliyo rahisi, basi jua hajui, anakudanganya au anataka kukutapeli.
Tabu iko pale pale, ikubali haraka na uifanyie kazi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed