2800; Ushahidi mwingine kwamba biashara siyo mtaji pekee.

Biashara kuu ya benki ni kutoa mikopo kwa watu, ambao watailipa kwa riba. Hivyo ndivyo benki zinaingiza faida.

Sehemu kubwa ya mikopo ambayo benki nyingi zinatoa ni ya biashara au uwekezaji.
Mtu anachukua mkopo kwenda kukuza zaidi biashara yake, kuongeza faida na kuweza kufanya marejesho.
Au mtu anachukua mkopo, anaenda kujenga nyumba ambayo atapangisha na kuweza kulipa mkopo huo.

Sasa hebu jiulize, kwa nini benki zisingekuwa zinafanya biashara zenyewe na kupata faida badala ya kuhangaika na kuwapa watu fedha hizo kama mkopo?
Kwa nini benki wakubali kusumbuka kuwadai watu walipe mikopo yao pale wanapochelewa kama wangeweza kufanya biashara husika peke yao?

Na hivi unajua benki zina wataalamu wote wa fedha, masoko, mauzo na uongozi, vitu ambavyo wangeweza kutumia kwenye biashara yoyote ile?

Je unadhani benki hazioni hizo biashara ambazo kila mtu anasema ni fursa na kukimbizana nazo?

Benki hazihangaiki na hayo yote kwa sababu zinajua biashara yao kuu ni moja tu, fedha.
Benki zina uelewa na ubobezi kwenye eneo la fedha.
Na zina mifumo mizuri inayoziwezesha kufanya biashara hiyo vizuri.
Na hayo ndiyo yanawezesha zifanikiwe kwenye hilo eneo.

Lakini nje ya eneo hilo la ubobezi, benki pamoja na wataalamu wake wote watapata shida kama watajiingiza kwenye kila aina ya biashara wanayosikia inalipa.

Na hapo ndipo inakuja sababu kwa nini watu wengi licha ya kuhangaika sana na biashara bado hawafanikiwi.
Kwa sababu kila wakati wanakimbizana na fursa mpya za biashara zinazojitokeza.
Kwa sababu tu wanaona wana mtaji, basi wanadhani wanaweza kufanya biashara yoyote.

Hilo linasababisha wasibobee kwenye biashara yoyote kwa kiwango cha kuweza kuifanya kwa ngazi ya juu.

Kila biashara ina fursa nyingi za mafanikio ndani yake.
Lakini fursa hizo hazitokei zenyewe, bali zinatengenezwa na anayefanya biashara hiyo.

Hivyo acha kufikiria biashara kama mtaji pekee. Jua kuna ujuzi, uzoefu, kazi na muda vinavyohitajika ili biashara iweze kufanikiwa.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini ni aina gani ya biashara unayotumia kujenga mafanikio yako makubwa. Haimaanishi itakuwa hiyo moja tu maisha yako yote, bali kila wakati utakuwa unajenga biashara moja mpaka ifikie mafanikio makubwa ndiyo uende kwenye nyingine unayotaka.

Tafakari;
Mtazamo wa kimafanikio wa watu ambao bado hawajafanikiwa ndiyo kikwazo kikuu kwao kufanikiwa. Usijiangalie wewe unavyofanya au wanavyofanya wale waliokuzunguka, ambao hamtofautiani sana. Badala yake waangalie wale waliofanikiwa zaidi yako wanavyofanya. Fanya kama wao na kwa hakika utafanikiwa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed