2801; Unaona nini ambacho wengine hawaoni?

Watu wawili, wenye uwezo sawa, wanaweza kuanza biashara ya aina moja na kwenye eneo moja, wakilenga wateja wa aina moja.

Baada ya muda, mmoja kati yao akawa amefanikiwa kuliko mwingine.
Je unadhani nini ambacho kinapelelea mmoja afanikiwe huku mwingine akishindwa?

Kumbuka wote wanaanzia ngazi sawa na hakuna anayepata upendeleo kumzidi mwingine.

Kitu kikubwa kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa, pale mazingira ya nje yanapofanana ni kile wanachoona.

Wanaofanikiwa kuna kitu wanaona, ambacho watu wengine hawakioni.
Wanakuwa na maono na ndoto kubwa, ambazo wanajiona kabisa wakiwa wamezifikia.
Maono hayo ndiyo yanayokuwa yanawaongoza kwenye kila wanachofanya na ndiyo yanapelekea wachukue hatua wanazochukua.

Wasiofanikiwa hawana kitu wanachoona ambacho wengine hawakioni. Hivyo mara zote wanafuata mkumbo wa kile wengi wanafanya.
Ni rahisi kubadilika kila wakati kwa sababu hakuna wanakokwenda.

Ukimkuta mchonga mawe akiwa anaanza kuchonga jiwe lake, unaweza kumcheka, kitakuwa kituko. Lakini picha ya kile anachotaka kufikia anakuwa nayo kwenye fikra zake.
Ni mpaka mwisho ndiyo wengine wanaona alichokuwa anakusudia.
Sasa pata picha kama mchonga mawe angekuwa anasikiliza ushauri wa kila mtu wakati anaanza kuchonga jiwe lake.
Kwa hakika angeishia kuwa na kitu cha ajabu kabisa, ambacho hakieleweki na yeyote.

Hivyo ndivyo maisha, kazi na biashara zilivyo. Kiwango chako cha mafanikio kinategemea sana picha unayoiona kwenye akili yako, ambayo hakuna mwingine anayeiona.
Kuiamini picha hiyo na kuisimamia ni nguzo muhimu ambapo mafanikio ya aina yote yanajengwa.

Ni maono makubwa unayokuwa nayo ndiyo yanayojenga mtazamo wako wa kifikra.
Na mtazamo unaokuwa nao ndiyo unaoathiri fikra zako na hatua unazochukua.
Hivyo chochote unachofanya, kinategemea sana picha kubwa uliyonayo ndani yako.

Hatua ya kuchukua;
Ni picha gani unaiona kwenye fikra zako ambayo watu wengine hawaioni? Andika chini maelezo ya picha hiyo na itumie picha hiyo kama mwongozo kwa kila unachofanya.
Kama hujui ni picha gani unayo, jiulize uko wapi miaka 10 ijayo, jione kabisa ukiwa pale unapotaka kuwa, kisha andika kila ulichonacho kwenye kipindi hicho.
Sasa rudi kwenye yale unayofanya kila siku, jiulize ni kwa namna gani yanakufikisha kwenye picha yako.
Kama jambo halina mchango, unaachana nalo, hata kama kila mtu analifanya.

Tafakari;
Mafanikio ni kuitoa picha ya ndani na kuileta kwenye uhalisia. Na hilo ndiyo limekuwa linaibadili dunia. Maendeleo yote tunayoyaona duniani, yalianza kama picha kwenye fikra za baadhi ya watu, ambao waliziamini licha ya wengine kutokuona picha hizo.
Usiue picha unayoiona kwenye akili yako, huwezi kujua ni kwa namna gani picha hiyo inaweza kuibadili dunia.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed