#SheriaYaLeo (306/366); Tumaini kwa ajili yetu wote.

Tumeshaona jinsi ambavyo sisi binadamu ni viumbe wa kihisia.
Huwa tunafanya maamuzi yetu kwa kusukumwa na hisia badala ya mantiki.
Na hilo ndiyo limekuwa chanzo cha matatizo ambayo tumekuwa tunakutana nayo kwenye maisha.

Lakini pamoja na hayo, bado lipo tumaini kwa ajili yetu wote.
Kuna mambo mawili makubwa yanayotupa tumaini.

Jambo la kwanza ni uwepo wa baadhi ya watu ambao waliweza kufanya makubwa hapa duniani kwa kutumia mantiki badala ya hisia.
Wamekuwa watu wa hekima na busara ambao wameweza kufanya maamuzi bora na ambayo yamewapa matokeo mazuri.
Kama wengine wameweza hilo ni dhahiri kwamba hata sisi tunaweza pia.

Jambo la pili ni uzoefu wetu wenyewe. Kila mmoja wetu kuna wakati kwenye maisha yake amewahi kujikuta ana wajibu mkubwa wa kukamilisha na hapo akaweka umakini wake wote kwenye wajibu huo bila kuruhusu hisia nyingine zozote kumwingilia.
Kwa jukumu kubwa linalokuwa mbele yako, huruhusu kitu kisichokuwa na tija kukukwamisha.
Kila mtu ana uzoefu kwenye hili na hicho ni kiashiria kwamba tunao uwezo wa kudhibiti hisia zetu na kufanya mambo kwa mantiki.

Mambo hayo mawili ambayo ni ya uhakika kabisa ni tumaini kubwa kwetu wote kwamba inawezekana kufanya mambo kwa mantiki badala ya hisia. Kwamba tunaweza kutumia hekima na busara kufanya makubwa.
Hivyo hatupaswi kujiona kama ndiyo hatufai kabisa, lipo tumaini, tunapaswa kulitumia vizuri.

Sheria ya leo; Hali tunazopitia ambapo tunaongozwa na mantiki badala ya hisia, hata kama ni fupi, bado ni kiashiria kwamba upo uwezo huo ndani yetu. Unachohitaji ni kulitambua hilo kisha kufanya mazoezi mengi ya kuweza kutumia zaidi mantiki kuliko hisia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji