2822; Umalaya wa fursa.

Richard Branson amewahi kunukuliwa akisema fursa za biashara ni kama daladala, ukikosa moja, kuna jingine linakuja.
Kwa maana rahisi ni kwamba fursa ni nyingi na haziishi.

Lakini wanachokifanya walio wengi ni kutaka kupanda kila daladala.
Pata picha umeenda kituo cha daladala, ikaja daladala ukaipanda, lakini kabla haijaondoka ikaja nyingine, ukashuka na kwenda kupanda hiyo.
Na yenyewe kabla ya kuondoka ikaja nyingine tena, ukashuka na kwenda kuipanda hiyo.
Ukaendelea na zoezi hilo bila kuacha, unadhani utafika wapi?

Jibu unalo, utabaki kwenye kituo hicho hicho. Licha ya kupanda daladala nyingi, hakuna hatua yoyote unayokuwa umeipiga.

Kama ungechagua kupanda kwenye daladala moja na kutulia hapo, kwa muda huo huo ungekuwa umepiga hatua, hata kama daladala hiyo inakwenda taratibu.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye fursa nyingi ambazo watu wanakutana nazo kwenye maisha.
Kukimbizana na kila fursa mpya inayokuja imekuwa ndiyo sababu kubwa ya wengi kushindwa kupiga hatua na kufanikiwa.

Inakuja fursa mpya, mtu anaiona ndiyo yenyewe hiyo, anaichagua na kuanza kuifanyia kazi. Mwanzo anaifurahia, lakini pale anapokutana na ugumu, badala ya kuukabili, anaona fursa nyingine nzuri zaidi na kwenda kuanza hizo, huku akiachana na ya mwanzo.
Mchezo unaenda hivyo, muda unakwenda na hakuna hatua anapiga.

Huo ndiyo umalaya wa fursa, kuhangaika na kila fursa mpya na kushindwa kuweka juhudi kubwa kwenye fursa moja kwa muda mrefu mpaka izae matunda.

Hatua ya kuchukua;
Chagua fursa moja ambayo utaifanyia kazi mpaka izae matunda unayotaka kabla hujahangaika na fursa nyingine.
Usiwe na tamaa ya fursa, ni nyingi na hazitakuja kuisha.
Unachotaka wewe ni kuzalisha matokeo yanayokufikisha kwenye kile unachotaka.

Tafakari;
Fursa ni nyingi na hakuna namna unaweza kuzimaliza zote. Chagua fursa moja ambayo utaifanyia kazi vizuri na kwa ukamilifu kabla hujaenda kwenye fursa nyingine.
Unaposhawishika na fursa mpya inayokuja mbele yako, jiulize kwanza kama ile unayofanyia kazi sasa umeshaimaliza yote.
Jibu ni nado, hivyo kabla hujatawanya nguvu zako, zikusanye kwenye fursa uliyonayo sasa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed