2828; Mteja mpya rahisi kumpata.

Hakuna kitu kigumu kwenye biashara kama kupata mteja mpya.

Kutokana na kudanganywa na kuumizwa kwa muda mrefu, wateja wana wasiwasi sana na biashara mpya kwao.

Ahadi nyingi unazowapa wanakuwa hawana uhakika kama kweli zitatimia.

Hilo ndiyo limekuwa linasababisha wasiwe tayari kununua, licha ya kuwa kuwapa maelezo mengi na uhakika wa kila aina.

Ni ugumu huu ndiyo umekuwa unawakatisha tamaa wafanyabiashara wengi na kuona ni bora waachane na kutafuta wateja wapya, badala yake waendelee kuwahudumia wateja waliopo.

Hilo siyo sahihi, wateja wapya lazima waendelee kutafutwa, na zipo njia nyingi bora za kukamilisha hilo.
Moja ya njia hizo ni rahisi na ya uhakika, ambayo ikitumika vizuri matokeo yake ni mazuri.

Njia hiyo ni kuwatumia wateja waliopo sasa kupata wateja wapya.
Wateja wapya ambao wameambiwa na watu wao wa karibu, huwa ni rahisi sana kuwashawishi wanunue.
Hiyo ni kwa sababu wana imani kwa wale waliowaambia na kuwa na uhakika watapata manufaa.

Ule ugumu wa wateja kukubali mwanzoni kwa sababu ya kukosa imani unakuwa umeondolewa na kitendo cha kuambiwa na watu wao wa karibu.

Kwa sababu wanajua watu hao hawana sababu ya kuwadanganya ili wanunue, na kwa sababu tayari wanawaamini, ugumu wa mwanzo unapungua kabisa.

Pamoja na njia hii kuwa rahisi, bado inahitaji mtu ufanye kazi kubwa sana.
Maana wateja hawatakuletea wateja wengine kama kweli hujawapa thamani.

Ni lazima kwanza uwape wateja thamani kubwa ndiyo wawe tayari kukuletea wateja wengine.

Lakini pamoja na kuwapa thamani kubwa, bado unapaswa kuwaomba wakuletee wateja wapya.
Na huwaombi tu vile unajisikia, bali unakuwa na mfumo sahihi wa kuwaomba, ambao utawawezesha kukupa wateja wapya.

Tumia wateja ulionao sasa kupata wateja wapya ambao watakuwa rahisi kuwashawishi.
Lakini kwanza wape huduma bora wateja hao kisha waombe wakupe kwa usahihi wakupe wateja wapya.

Hatua ya kuchukua;
Pitia wateja wote ulionao sasa kwenye biashara yako. Chagua wale walioridhika hasa na kile wanachopata kwako. Mwombe kila mmoja akutajie watu wawili anaowajua ambao wanaweza kunufaika na biashara yako kama wao. Kisha waombe wakupe mawasiliano yao na wawasiliane nao kuwajulisha thamani wanayoweza kupata kwako. Watafute wateja hao na uwakamilishe kuwa wateja kamili.
Ukifanya zoezi hili vizuri na kwa msimamo, utaweza kupata wateja wengi na kwa uhakika.

Tafakari;
Wateja ulionao sasa kwenye biashara yako ni mgodi wa dhahabu. Ukiwatumia vizuri utaweza kupata wateja wengine wengi na kwa urahisi.
Anza kwa kuwahudumia vizuri ulionao na waombe kwa usahihi wakupe wateja wapya.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed