2829; Kuwaona huruma wasiojionea huruma.

Changamoto zetu kubwa kwenye maisha zinatokana na watu.
Ni changamoto kubwa kwa sababu tunawahitaji sana watu, lakini ndiyo hivyo wanakuja na mambo yao ambayo yanatupa changamoto.

Kwa kuwa tunawahitaji sana watu, kuna wakati tunakuwa hatutaki kuwapoteza, hivyo licha ya chagamoto wanazosababisha, tunaendelea kuwa nao.

Na kuna wale ambao licha ya changamoto wanazokuwa nazo, bado tunaendelea kuwa nao kwa sababu tunawaonea huruma.

Kwa kuanza, nieleze wazi kwamba kama unakaa na watu wanaokusababishia changamoto, unastahili hilo unalopitia.

Kwa sababu ukisema huwezi kupata wengine hilo siyo kweli, watu sahihi wapo wengi tu.
Ni wewe hujaweza kuwafikia na kuwashawishi ushirikiane nao.

Na kama unaendelea kukaa na wanaokupa changamoto kwa sababu unawaonea huruma, hilo pia ni kujipa matumaini hewa tu.
Kwa sababu unamuonea huruma mtu ambaye yeye mwenyewe hajionei huruma.

Kama mtu anakuletea changamoto, unamweleza wazi kuhusu hilo, lakini bado anaendelea kusababisha changamoto, unadhani anajionea huruma yeye mwenyewe?

Twende kwenye mfano kabisa, una mfanyakazi, ambaye kila wakati anachelewa kazini, umeshamkanya sana lakini bado hilo halikomi, unadhani yeye mwenyewe anajionea huruma?
Jibu ni hapana, hajionei huruma.
Hivyo kama wewe unamwonea huruma, ni kutaka tu kujipa matumaini wewe binafsi na siyo kumsaidia mfanyakazi huyo.

Kwa hakika tunaweza kusema, mfanyakazi aliyeichoka kazi au ambaye haithamini, huwa anaomba yeye mwenyewe kufukuzwa.
Haombi waziwazi, bali kwa vitendo. Kuna mambo ambayo atakuwa anayafanya kwa makusudi kabisa, iwe kwa kujua au kutokujua, lakini hitaji lake ni kazi hiyo isiendelee kuwepo kwenye maisha yake.

Sasa kwa wewe kumng’ang’ania, kwa kigezo cha kumwonea huruma, humsaidii na unajibebesha mzigo zaidi.

Sisemi usiwe na huruma, nasema waonee huruma wale ambao wanajionea huruma. Wale wasiojionea huruma, wape kile wanachostahili.

Hatua ya kuchukua;
Pitia watu wote unaojihusisha nao moja kwa moja.
Ainisha wale ambao wanakuletea changamoto mbalimbali.
Pitia kila changamoto na angalia ni zipi unaendelea kuzibeba kwa kuwaonea huruma watu ambao hawajionei huruma wao wenyewe?
Kama changamoto za aina hiyo zipo, chukua hatua za mara moja kuwapa kile wanachostahili.

Tafakari;
Huruma ni nzuri kwenye maisha pale inapoelekezwa kwa watu sahihi, ambao pia wanajionea huruma. Kuwahurumia ambao hawajihurumii ni kutengeneza changamoto ambazo zitakusumbua sana.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed