2832; Gharama ya kuepuka watu wa kawaida.
Ili ufanikiwe, unawahitaji sana watu.
Lakini watu hawalingani.
Kuna watu wa kawaida, ambao ndiyo wengi. Hawa pia ni rahisi kuwapata.
Halafu kuna watu wasio wa kawaida, ambao ni wachache na wagumu kuwapata.
Ili upate mafanikio makubwa, unahitaji kuwaepuka watu wa kawaida na kuwapata wasio wa kawaida.
Hilo ndiyo limekuwa zoezi gumu kwa wengi na linalowazuia wasifanikiwe.
Wengi wamekuwa hawapo tayari kulipa gharama ili kupata watu sahihi.
Badala yake wanapokea wale wa kawaida wanaopatikana kirahisi na ambao hawawezi kuwaletea matokeo ya tofauti.
Kupata wateja bora kwenye biashara yako, lazima uingie gharama ya kuwafikia kule walipo na kuwashawishi wanunue kwako.
Hawa siyo wateja rahisi kupatikana kama wa kawaida, lakini faida yao ni kubwa zaidi.
Kupata wafanyakazi bora kwenye biashara yako, lazima uingie gharama kuwatafuta, kuwalipa na hata kuwaendeleza. Hawa siyo wafanyakazi rahisi kuwapata kama wa kawaida, lakini ukiwapata, thamani wanayokupa ni kubwa pia.
Kuwaepuka watu wa kawaida, ambao ndiyo wamekuzunguka kwa wingi kunahitaji gharama.
Kama haupo tayari kulipa gharama hizo, utaishia kukubali watu wa kawaida ambao watakuchelewesha kufanikiwa.
Mafanikio yako yanahitaji sana watu ambao siyo wa kawaida. Kuwapata watu hao kuna gharama yake, lakini ni gharama zinazojilipa vizuri baadaye.
Hatua ya kuchukua;
Chunguza kila eneo la maisha yako na jiulize ni watu wa aina gani unao, wa kawaida au wasio wa kawaida. Kama wengi ni wa kawaida, jua unatafuta urahisi ambao unakugharimu zaidi. Ni bora uweke gharama kuwapata watu sahihi na hao watakuwezesha kupiga hatua kubwa.
Tafakari;
Hakuna jeshi la mtu mmoja. Lakini pia siyo kila jeshi linashinda vita. Ushindi wa vita unategemea sana uimara wa jeshi. Na uimara wa jeshi unategemea na uwekezaji uliofanyika.
Fanya uwekezaji wa kupata watu wasio wa kawaida kwenye kila eneo la maisha.
Ni uwekezaji utakaokulipa sana.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed
Asante sana mkuu kww hili,,,
LikeLike
Karibu
LikeLike